Monday, 24 October 2016

WALIOPATA MAJANGA YA MOTO KUTIBIWA BURE AGA KHAN

Image result for agakhan hospital dar es salaam
HOSPITALI ya Aga Khan ya jijini Dar es Salaam, inatarajia kufanya uchunguzi na kutoa matibabu ya bure ya upasuaji wa kurekebisha viungo kwa wanawake na watoto wa kike ambao wameathirika na kupata ulemavu uliotokana na vurugu, majanga ya moto na ajali mbalimbali.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, Meneja Miradi wa hospitali hiyo, Nasreen Hassanal alisema uchunguzi huo wataufanya Oktoba 29 mwaka huu kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 7:00 mchana.
Uchunguzi huo utafanywa na madaktari bingwa kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili na kwa watakaobainika kuwa na matatizo baada ya uchunguzi huo watafanyiwa upasuaji bure.
Alisema uchunguzi huo unafanywa kupitia 'Women for Women' na walengwa ni wanawake wote na watoto wote wa kike wenye makovu yaliyotokana na ajali mbalimbali ambao watafanyiwa upasuaji wa kurekebisha viungo vyao bila malipo.
"Tumetenga Sh milioni 125.5 kwa ajili ya kazi hiyo na kwa kawaida gharama za upasuaji mkubwa kwa mgonjwa kama huyo ni Sh milioni 2.5 na gharama za upasuaji mdogo ni Sh milioni 1.75," alisema.
Alisema kwa Januari mwaka huu walifanya uchunguzi mwingine kama huo na kuwafanyia upasuaji wanawake na watoto wa kike 35, ambao 30 kati yao walikuwa na majeraha makubwa na watano walikuwa na majeraha madogo.
"Kwa wanaobainika wana matatizo, tunawafanyia vipimo vyote bure, upasuaji wa bure na hatimaye tunamuweka kwenye uangalizi kwa muda hadi afya zao zinapoimarika," alisema.
Alisema kwa siku hiyo wanatarajia kupokea watu zaidi ya 250 na watachagua wagonjwa ambao wanastahili kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha viungo.
Alisema baada ya uchunguzi huo kukamilika vipimo vingine vitafanyika Desemba 8 na upasuaji utafanyika Desemba 9 hadi 11 na Desemba 12, itakuwa ni uangalizi wa maendeleo ya wagonjwa.
HABARI LEO:

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!