SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema kero mbili kati ya tatu za mambo ya Muungano zimetatuliwa na serikali ya awamu ya tano tangu Rais John Magufuli aingie madarakani, mwaka huu.




Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed, alitoa msimamo huo jana alipokua akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu hatua zilizofikiwa katika utatuzi wa kero za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Aboud alisema, baada ya vikao viwili vya kisekta kufanyika chini ya uongozi wake, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kero mbili zimepatiwa ufumbuzi na moja inaendelea kufanyiwa kazi na watendaji.
Alisema kuanzia sasa vyombo vya moto vilivyosajiliwa Tanzania Bara yakiwamo magari na namba zake ni ruhusa kutumika Zanzibar na utaratibu kama huo kutumika kwa magari yaliyosajiliwa Zanzibar na kutumika upande wa Tanzania Bara.
“Vyombo vya moto yakiwamo magari yanaruhusiwa kutumika pande mbili za Muungano ila jambo la muhimu yawe yamesajiliwa kwa mujibu wa sheria,” alisema Waziri Aboud.
Aidha, alisema kuanzia sasa mfumo wa ulipaji kodi ya Ongezeko la Thamani Tanzania (VAT), umebadilika, bidhaa zinazozalishwa Tanzania Bara na kuingia soko la Zanzibar, zitalipiwa Zanzibar badala ya Tanzania Bara na utaratibu kama huo utumika kwa bidhaa zinazozalishwa Zanzibar na kulipiwa Tanzania Bara.
“Kabla ya mabadiliko hayo, Mamlaka ya Kodi ya Mapato Tanzania (TRA) ilikuwa wakala wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) na ilikusanya kodi ya VAT kwa bidhaa zinazozalishwa Tanzania Bara na kuingizwa Zanzibar,”alifafanua Waziri huyo.
Alisema kimsingi kero za Muungano zimetatuliwa kwa kiwango kikubwa na kero hizo tatu zilikuwa ndiyo zimebaki kiporo baada ya mambo mengi kuzingatiwa katika mabadiliko ya Katiba inayopendekezwa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema kero moja ya mgawo wa mapato kupitia faida ya ya Benki Kuu ya Tanzania inaendelea kufanyiwa kazi baada ya watendaji wakuu kutakiwa kupitia nyaraka mbalimbali kabla ya kufikiwa kwa mwafaka wake.
Alisema Zanzibar imekuwa ikinufaika na gawio la asilimia 4.5 na kueleza kuwa Tume ya Pamoja na Fedha, imepitia vyanzo vya
mapato ya Muungano na ripoti yake inaendelea kufanyiwa kazi kwa madhumuni ya kuimarisha Muungano.

Hata hivyo, alisema mapato yote yaliyokusanywa Zanzibar na Mamlaka ya Kodi ya Mapato Tanzania (TRA), yamekua yakibaki
Zanzibar na kutumika kwa shughuli za maendeleo na huduma za jamii kwa wananchi wake kinyume na madai yanayoenezwa na wapinzani visiwani Zanzibar.
Alisema Zanzibar ndiyo imekua ikipata unafuu kutokana na gharama za uendeshaji na TRA Zanzibar malipo ya mishahara ya wafanyakzi hugharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

NIPASHE.