Friday, 21 October 2016

MTUMBWI WAPASUKA NA KUUA WATATU

WAVUVI watatu wamekufa katika bwawa la Masoghweda lililopo kata ya Ikhanoda, Ilongero wilayani Singida baada ya mtumbwi waliokuwa wakitumia kuvulia samaki kupasuka na wao kuzama.


Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Mayala Towo aliwataja waliokufa kuwa ni Rajabu Mohammed (21), Miraji Rajabu (24) na Onesmo Emmanuel (20) wote wakazi wa kijiji cha Masoghweda wilayani humo.
Towo alisema wakati miili ya Mohamed na Rajabu imeshakabidhiwa kwa ndugu zao kwa maziko, mwili wa Emmanuel haujapatikana.
Alisema mjini hapa jana kuwa tukio hilo ni la juzi mchana ambapo miili hiyo iliopolewa siku hiyo hiyo baada ya Jeshi la Zimamoto kusaidia.
Hata hivyo, alisema hadi sasa sababu za kupasuka mtumbwi huo hazijafahamika ingawa uchunguzi wa awali unaonesha kuwa huenda ulikuwa umebeba mzigo mkubwa kuzidi uwezo wake.
Wakati huo huo, walimu wanane wa shule ya msingi Sekenke wamenusurika kifo baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugonga kingo za barabara kuu ya Misigiri – Igunga baada ya breki za gari hilo kushindwa kufanya kazi eneo la mlima Sekenke.
Aliwataja walimu hao kuwa ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Sekenke, Ibrahimu Mlula aliyekuwa akiendesha gari hilo aina ya Suzuki lenye namba za usajili T.130 AEW, Basil Mkome na Oliva Mkude. Wengine ni Shadrack Suda, Evelin Lema, Felista Godluck, Zawadi Palangyo na Sosthenes Videlius.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!