SERIKALI imeahidi kuboresha na kuimarisha maslahi kwa watumishi wote wa umma kupitia Bodi ya Mishahara na motisha mara watakapokamilisha uhakiki wa taarifa za kiutumishi kwa wafanyakazi wa umma, ambao utawezesha kupanga upya mishahara na motisha kwa watumishi.
Aidha, imesema italipa madeni yote inayodaiwa na watumishi wake wote mara itakapomaliza kufanya uhakiki huo ili kubaini watumishi hewa.
Ahadi hiyo ilitolewa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm).
Katika hotuba yake, Majaliwa alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuhakikisha inaondoa malimbikizo ya madai kwa watumishi wote wa umma, na mojawapo ya mikakati hiyo ni uhakiki, ambao unaendelea wa watumishi wa umma. Alisema hadi Oktoba 20, mwaka huu watumishi hewa, ambao wamebainika kutokana na uhakiki huo walikuwa ni 16,500.
“Baada ya uhakiki huo tutarudia uhakiki wa madeni yote yaliyowasilishwa serikalini na kisha tutalipa madeni ya watumishi wote yakiwemo madeni yanayodaiwa na wanataaluma,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Kwa muda mrefu sasa, serikali inaendesha uhakiki wa watumishi wa umma baada ya kubainika kuwapo na watumishi hewa wengi wanaolipwa fedha nyingi kila mwezi, hivyo kuipotezea mapato serikali ambayo yangetumika kwa kazi nyingine, zikiwamo za kuboresha mishahara ya watumishi na huduma za kijamii.
Akizungumzia changamoto zinazokikabili Chuo Kikuu cha Dar es Salam likiwemo suala la uhaba wa wahadhiri waandamizi pamoja na tatizo la mikopo kwa wanafunzi, Majaliwa alisema serikali itaendelea kuweka kipaumbele cha upatikanaji wa fedha za kutosha kwa ajili ya mafunzo.
Lakini, pia amevitaka vyuo vya umma, kuhakikisha taratibu na mipango endelevu ya kurithishana kwani bila kufanya hivyo wakati wote kutakuwa na mapungufu katika utoaji wa taaluma. Alisema serikali itaendelea kuwaajiri wanataaluma na watumishi wengine wapya pale wanapohitajika.
Alitoa ahadi hiyo baada ya kuelezwa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala kuwa chuo hicho kwa sasa kinakabiliwa na uhaba mkubwa wa wahadhiri waandamizi kutokana na wengi wao kustaafu.
Kuhusu changamoto ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, Majaliwa alisema Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi inaendelea kufanya uhakiki wa taarifa za waombaji wa mikopo na akasema kufikia kesho asilimia 90 ya waombaji ambao wametimiza masharti watakuwa wameshalipwa fedha zao.
Aliwataka watumishi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kutimiza wajibu wao kuhakikisha kwamba, kwa wale ambao uhakiki wao umekamilika wapatiwe mikopo hiyo kwa wakati. Alisema kamwe serikali haitawavumilia watumishi ambao watachelewesha kwa makusudi mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
“Kama kuna taarifa itolewe ndani ya serikali haraka ili ifanyiwe kazi kuzuia mgogoro kati ya wanafunzi na serikali yao,” alisema Majaliwa.
Awali, Profesa Mukanda alisema changamoto kubwa inayokikabili chuo hicho kwa sasa ni uhaba wa wanataaluma waandamizi katika fani mbalimbali tatizo ambalo alisema linatokana na serikali kusitisha ajira kwa miaka 10 na hivyo kutoajiriwa wanataaluma chipukizi.
Alisema hali ilivyo kwa sasa katika vyuo vya umma nchini ni mamia ya wanataaluma wazoefu kustaafu kwa wakati mmoja na wanataaluma walioajiriwa katika miaka ya hivi karibuni, bado wako masomoni au wangali chipukizi katika taaluma zao na hivyo kutokuwa na uwezo wa kutosha kubeba majukumu ya kufundisha shahada za umahiri na uzamivu.
Alisema licha ya serikali kuruhusu utoaji wa ajira za mikataba kwa wanataaluma wanaostaafu, lakini bado idara nyingi zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa wanataaluma waandamizi.
Alisema hali hiyo inatishia kukwamisha utekelezaji wa azma na mpango mkakati wa chuo hicho ambao ni kupanua programu za mafunzo ya digrii katika ngazi za umahiri na uzamivu.
Kwa hali hiyo aliiomba serikali kutoa mwongozo utakaosaidia vyuo vikuu vya umma vinavyokabiliwa na changamoto hiyo ili viweze kuepuka hatari iliyopo ya kushuka kwa viwango ya utoaji maarifa.
“Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kiko tayari kutoa mchango wa mawazo kuhusu namna ya kuruka kizingiti hicho,” alieleza.
No comments:
Post a Comment