Thursday, 20 October 2016

MAADHIMISHO YA MIAKA 71 YA UMOJA WA MATAIFA YASISITIZA MALENGO YA MAENDELEO ENDELEVU



’Wito watolewa kwa kila mwananchi kuwajibika kwa malengo ya Dunia’

OKTOBA 24 kila mwaka Umoja wa Mataifa hufanya maadhimisho ya kuzaliwa kwake.

Mwaka huu mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania kwa kushirikiana na serikali, wadau wa maendeleo na vijana wataadhimisha miaka 71 ya uwapo wa Umoja wa Mataifa kwa staili ya aina yake.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa katika mkutano wa waandishi wa habari na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikishirikiana na Umoja wa Mataifa , maadhimisho hayo mwaka huu yamelenga kuelezea kwa undani shughuli zinazofanywa kwa pamoja kati ya pande hizo mbili ili kuwezesha maendeleo endelevu.

Katika mkutano huo wa pamoja, waandishi wa habari walielezwa kwa ufupi Mpango Mpya wa Maendeleo Chini ya Ufadhili wa Umoja wa Mataifa ( UNDAP ll -2016 hadi 2021) kwa serikali ya Tanzania; na mpango wa maendeleo wa miaka mitano wa Tanzania ambamo malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) kama yalivyosanifiwa na kukubalika na jumuiya ya kimataifa, yameshirikishwa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Mhe. Balozi Dkt. Mahiga, amezungumzia umuhimu wa maadhimisho wa Siku ya Umoja wa Mataifa na faida za Jukwaa la umoja huo kwa maendeleo ya Taifa. Maadhimisho hayo yatafikia kilele tarehe 24 Oktoba, 2016.(Picha zote na Reginald Kisaka wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki).

Katika mkutano huo na waandishi wa habari pia kulikuwepo na majadiliano ya mafanikio ya shughuli za Umoja wa Mataifa hadi sasa duniani na pia nchini Tanzania .

Pia mazungumzo hayo yalijikita katika malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na umuhimu wa malengo hayo kumilikishwa kwa wananchi na wajibu wao katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na utekelezaji wenye mafanikio.

Pia ilielezwa katika mkutano huo kwamba maadhimisho ya miaka 71 ya Umoja wa Mataifa, Siku ya Umoja wa Mataifa, yatafanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam Oktoba 24.

Maadhimisho hayo ambayo mwaka huu yamebeba ujumbe wa :“Uwezeshaji wa vijana Tanzania kufikia malengo ya dunia” yanafanyika huku kukiwa na malengo mapya ya dunia ya maendeleo endelevu.Malengo hayo ya SDGs yamelenga kuondoa umaskini kwa kuwa na maendeleo endelevu.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga katika mkutano na waandishi wa habari.

Aidha ujumbe huo unaenda sanjari na mpango wa maendeleo wa awamu ya pili wa Umoja wa Mataifa kwa Tanzania (UNDAP II) ambao unaendeleza ule wa awali wa kuanzia 2011-16 ukiwa umejikita katika masuala ambayo ni muhimu kwenye kukabili umaskini kwa kuwa na maendeleo endelevu.

Maadhimisho ya mwaka huu yalitanguliwa na kongamano la vijana wapatao 200, ambao walijadili masuala yanayogusa fursa za uchumi na maendeleo ya jamii na mchango ambao unaoweza kutolewa na vijana kufanikisha utekelezaji wa malengo hayo.

Maadhimisho hayo yatafikia kilele chake nchini kwa tukio litakalofanyika Visiwani Unguja Oktoba 26 mwaka huu.

Imeelezwa kuwa maadhimisho ya mwaka huu yanaonesha uwapo wa ushirikiano mkubwa na wenye tija kati ya Tanzania, wananchi wake na Umoja wa Mataifa.
Kaimu Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Bi.Chansa Kapaya akizungumza na waandishi wa habari.

Aidha maadhimisho hayo yanaonesha ni kwa namna gani pande zote zipo tayari kutekeleza mipango ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania yenye lengo la kusaidia utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu.

Akizungumza umuhimu wa ushirikiano huo katika kutekeleza mpango wa maendeleo wa miaka mitano, ukiwa ni mpango wa wananchi wenyewe, Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw Augustine Mahiga, alielezea Tanzania kuunga mkono Umoja wa Mataifa ukifanyakazi kama taasisi moja na kuwataka watengeneza sera kuhakikisha kwamba wananchi wote wananufaika na ushirikiano huu wa Tanzania na Umoja wa Mataifa.

Waziri Mahiga alisisitiza wakati Tanzania inajikita katika kutekeleza mpango wake mpya wa taifa wa maendeleo, kuna haja ya kuhakikisha kwamba wananchi wanaelewa na kumiliki mpango huo ambao umejumuisha malengo ya maendeleo endelevu.
Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy (kushoto) akifuatilia mkutano. Kulia ni Kaimu Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Bi.Chansa Kapaya.

Alisema: “Tanzania imeshirikisha malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) katika sera za taifa na pia katika mipango ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo ya msingi yanayohitaji uangalizi kufanikisha maendeleo endelevu”. 

Hata hivyo aliongeza kusema kwamba: “ Hiyo inajulikana wazi kwamba serikali pekee haiwezi kufanikisha utekelezaji wa ajenda ya maendeleo endelevu bila msaada wa sekta binafsi na wadau wetu wa maendeleo, na hivyo iko haja ya kushirikishana. Tunaitaka sekta binafsi na wadau wetu wa maendeleo kujiunga nasi katika juhudi hizi kwa kutuwezesha kifedha ili tuweze kutekeleza mipango yetu ya maendeleo. Tunachohitaji sisi tunaofanyakazi katika ushirikiano wa kimataifa kuhakikisha kwamba hatutamwacha yeyote nyuma katika harakati zetu za kuleta maendeleo”.

Naye Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Bw. Alvaro Rodriguez akizungumzia maadhimisho ya miaka 71 ya Umoja wa Mataifa na uhusiano wake alisema: “Tanzania na Umoja wa Mataifa zimekuwa na ushirikiano wa maendeleo kwa miongo mingi. Wakati Tanzania sasa inabadilika, msaada unaotolewa na Umoja wa Mataifa unatakiwa kukidhi haja mpya, hasa taifa linapoelekea katika uchumi wa kati”.

Pia katika hotuba yake aliongeza kwamba: “Malengo ya maendeleo endelevu ni muhimu katika ushirikiano wetu kwani unaweka umuhimu wa shughuli za Umoja wa Mataifa nchini Tanzania za kusaidia kupatikana kwa mafanikio katika nyanja za uchumi, ustawi wa jamii na utunzaji wa mazingira.”

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!