Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema Kenya ni nchi inayoongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania ikilinganishwa na nchi nyingine za Bara la Afrika.
Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 31 Oktoba, 2016
katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika
katika Ikulu ya Nairobi nchini Kenya ambako ameanza
ziara ya Kiserikali ya siku mbili kwa mwaliko wa Rais
wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta.
Rais Magufuli ambaye kabla ya Mkutano huo na waandishi wa habari amepokelewa rasmi kwa kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa heshima yake na baadaye kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta, amesema takwimu za kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonesha kuwa Kenya ina jumla ya kampuni 529 zinazoendesha shughuli zake nchini Tanzania ambapo zimewekeza Dola za Marekani Bilioni 1.7 na zimeajiri watu 56,260.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akikagua gwaride la heshima aliloandaliwa na Jeshi la Kenya mara baada ya kuwasili katika Ikulu ya Nairobi nchini Kenya.
Pia, Rais Magufuli amebainisha kuwa biashara kati ya Tanzania na Kenya imeongezeka kutoka Shilingi za Kitanzania Bilioni 652.9 hadi Shilingi za Kitanzania Trilioni 2.044.
"Naomba niwahakikishie kuwa uhusiano na ushirikiano wetu ni mzuri na utaendelea kuwa mzuri zaidi, na kwetu sisi Tanzania, Kenya ndio nchi ya kwanza kwa uwekezaji kuliko nchi zote za Afrika.
"Tunashirikiana vizuri katika uchumi, watu wetu wanafanya kazi pamoja, yapo makabila yetu ambayo yanaingiliana kwa shughuli zao za kila siku na hata wanyamapori wetu wanazunguka katika nchi zote mbili bila kujali mipaka" amesema Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli amesisitiza kuwa Serikali yake itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na Kenya ulioasisiwa na Rais wa Kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa Kwanza wa Kenya Hayati Mzee Jomo Kenyatta na amewakaribisha wafanyabiashara wengi zaidi wa Kenya kuwekeza nchini Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisali mbele ya kaburi la Muasisi na Rais wa Kwanza wa Kenya Maremu Mzee Jomo Kenyatta mara baada ya kuweka shada la maua katika eneo la katikati ya jiji la Nairobi nchini Kenya mara baada ya kuwasili nchini humo
"Kabla ya kuja hapa nimekwenda kutoa heshima katika kaburi la Mzee Jomo Kenyatta, kwa kweli nimeguswa sana na kazi kubwa iliyofanywa na wazee wetu, naomba niwahakikishie kuwa tunawathamini sana ndugu zetu Wakenya na tutaendelea kufanya hivyo" amesisitiza Dkt. Magufuli.
Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta amemshukuru Rais Magufuli kwa kukubali mwaliko wake na amemhakikishia kuwa Kenya itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano na Tanzania.
"Kwetu sisi Tanzania ni ndugu zetu, ni kaka na dada zetu tunao ushirikiano wa siku nyingi na wa kidugu na tutahakikisha tunauendeleza ushirikiano na uhusiano huu mzuri ulioasisiwa na wazee wetu" amesema Mhe. Kenyatta.
Rais Kenyatta amesema Tanzania na Kenya ni nchi zinazofanana kwa mambo mengi muhimu ikiwemo kubadilishana uongozi wa Serikali kwa njia ya amani na ameongeza kuwa katika mazungumzo yao wamekubaliana kuwa nchi hizi zitaendelea kuzisaidia nchi nyingine za Afrika Mashariki zinazokabiliwa na matatizo mbalimbali.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo na mwenyeji wake Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta mara baada ya kumaliza mazungumzo yao katika Ikulu ya Nairobi nchini Kenya.
Aidha, Rais Kenyatta amesema Kenya itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi ya ushirikiano ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama vile barabara ya Bagamoyo (Tanzania) hadi Malindi (Kenya) pamoja na mambo mengine ambayo Tume ya pamoja ya ushirikiano kati ya nchi hizi mbili (Joint Commission Cooperation) itayaainisha.
Baadaye leo, Rais Magufuli anatarajiwa kuhudhuria dhifa ya kitaifa katika Ikulu ya Nairobi aliyoandaliwa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta na Kesho anatarajiwa kutembelea kiwanda cha maziwa cha Eldoville kilichopo Karen Jijini Nairobi, na kuzindua barabara mchepuko ya Southern By-pass iliyopo Jijini Nairobi.
No comments:
Post a Comment