Wednesday, 19 October 2016

JPM amfuta kazi DED aliyemtisha trafiki

RAIS John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, Emmanuel Mkumbo siku moja baada ya kufikishwa mahakamani kwa makosa ya usalama barabarani pamoja na kutishia kumuua kwa bastola askari wa usalama barabarani.


Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jana kwa vyombo vya habari, Rais Magufuli ametengua uteuzi huo kuanzia Oktoba 18, 2016.
“Uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga atakayejaza nafasi ya Emmanuel Mkumbo utafanywa baadaye,” ilieleza taarifa ya Ikulu.
Julai 7, mwaka huu, Rais Magufuli alifanya uteuzi wa wakurugenzi wa halmashauri za majiji matano, manispaa 21, miji 22 na wilaya (DC) 137 za Tanzania Bara.
Katika uteuzi huo uliotangazwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mussa Iyombe, kati ya wakurugenzi wote 185 walioteuliwa, 65 wameteuliwa kutoka orodha ya wakurugenzi wa zamani na 120 ni wakurugenzi wapya, akiwamo Mkumbo aliyepangiwa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga.
Juzi, Mkumbo (41) alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro kwa tuhuma za kumtishia kumuua kwa bastola askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani humo pamoja na kuvunja sheria za usalama barabarani.
Mkumbo, ambaye ni mkazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam, alipandishwa kizimbani na alisomewa mashtaka hayo na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Sunday Hyera, akisaidiana na Ediga Bantulaki mbele ya Hakimu Agripinas Kimanze.
Kwa mujibu wa waendesha mashitaka hao wa serikali, mtuhumiwa huyo anakabiliwa na kesi mbili, ya kwanza ikiwa ni kesi ya jinai kifungu cha 226 ya mwaka 2016 na ya pili ni kesi ya Usalama Barabarani Kifungu cha 222.
Mtuhumiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Oktoba 15, mwaka huu, eneo la Mkambarani Wilaya ya Morogoro katika barabara kuu ya Morogoro-Dar es Salaam wakati akiendesha gari aina ya Toyota Pajero yenye namba za usajili T 845 CTJ.
Kosa la kwanza linalomkabiri Mkurugenzi Mtendaji huyo ni kutishia kumuua kwa bastola askari aliyejulikana kwa jina la Koplo Titunda, akiwa katika majukumu yake ya kikazi na makosa mengine ni kuendesha gari lenye namba T845 CTJ aina ya Toyota Pajero bila ya kuwa na leseni na kuendesha gari bila bima.
Hyera alidai kuwa makosa mengine ni mwendo kasi katika eneo lililoruhusiwa kuendesha mwendo wa spidi 50 kwa saa, lakini alivuka na kufikia 85, kugoma kupeleka gari kituo cha Polisi na kuendesha bila kuwa na uangalifu barabarani.
Mtuhumiwa huyo alikana makosa hayo na kuachiwa kwa dhamana, huku kesi yake ikitarajiwa kufikishwa tena mahakamani hapo Oktoba 31, mwaka huu, Hata hivyo, jitihada za waandishi wa habari kupata picha ya mtuhumiwa hazikufanikiwa baada ya askari kumziba mtuhumiwa kwa koti pamoja na kofia aina ya pama na kumuingiza katika gari aina ya Toyota na kutokomea naye.

HABARI LEO.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!