AJALI ya barabarani ya basi la kampuni ya Power Toll lililokuwa likitokea Nakonde mpakani mwa Tanzania na Zambia likielekea Lusaka, inapaswa kutuachia fundisho la kujenga utamaduni wa kutembelea na vitambulisho.




Katika ajali hiyo, watu 22 walipoteza maisha, wakiwamo Watanzania wanne huku wengine 38 wakipata majeraha, baada ya basi hilo kupinduka nchini Zambia karibu na mpaka wa Tanzania katika mkoa wa Songwe.
Kitu cha kusikitisha ni kwamba kati ya Watanzania wanne waliofariki dunia, mmoja wao hakutambulika kutokana na kutokuwa na utambulisho (kitambulisho) na kuwa vigumu hadi sasa mwili wake kuurejesha nchini.
Watatu waliotambuliwa kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe, Mathius Nyange, ni Elias Songa (44), Huruma Ibingira (33) na Lusajo Mwambapa, wote wafanyabiashara na wakazi wa Tunduma mkoani Mbeya.
Alichokibainisha Kamanda Nyange ni kwamba Watanzania wengi wana tabia ya kusafiri kwenda umbali mrefu bila kuwa na vitambulisho na kwamba hilo limekuwa ni tatizo kubwa.
Kwamba wengi wamekuwa wakisafiri kwa njia za panya, kitendo ambacho si kizuri yanapotokea matatizo zikiwamo ajali. Angalizo la Kamanda Nyange linapaswa kuwa changamoto kwa Watanzania wote kwa sababu wengi wana tabia ya kusafiri bila kuwa na vitambulisho hata kuingia nje ya mipaka yetu kwa njia za kificho.
Kitambulisho ndiyo alama ya kumtambua anapotakiwa kutambuliwa kwa mabaya au mazuri, hivyo ni lazima kwa kila mtu kutembea na kitambulisho. Kuna aina yingi za vitambulisho vinavyotambuliwa kama cha mpigakura, cha taifa, cha ajira, leseni ya udereva, benki na mifuko ya hifadhi ya jamii.
Katika mazingira kama ya iliyotokea ajali hiyo ndani ya Zambia na mpaka wa Tanzania, baadhi ya Watanzania kutokuwa na vitambulisho matokeo yake ni hayo ya baadhi kushindwa kutambuliwa kwa ajili ya miili kurejeshwa na kupatiwa matibabu.
Inawezekana kuwa miongoni mwa majeruhi 38 wa ajali hiyo walipelekwa katika hospitali ya mkoa Zambia kwa matibabu, wamo Watanzania, ambao kwa vyovyote vile watahitaji kuwa na pasi za kusafiri kabla ya kupata huduma za matibabu na kurejeshwa nchini.
Kutembea na vitambulisho unapaswa kuwa utamaduni wa kila mmoja pale anapoondoka nyumbani kwake kwenda sehemu nyingine kwa kuwa wakati wowote anaweza kutakiwa kukionyesha.
Kwa mfano, kuna mazingira ambayo polisi wanaweza kuwa katika msako wa wahalifu au wahamiaji haramu na kumtaka kila mmoja kutoa kitambulisho ili wajiridhishe kuwa ni raia mwema. Kwa kushindwa kuonyesha kitambulisho, mtu wa aina hiyo anaweza kujikuta anapata usumbufu ikiwamo kukamatwa na kulala polisi.
Kuna baadhi ya maeneo ya mipaka yetu ambayo Watanzania wanaoishi hapo wameshajenga utamaduni wa kuingia nchi jirani bila pasi za kusafiria kutokana na mwingiliano wa kila siku unaosababisha raia wa nchi hizo kuzoeana. Maeneo mengine ya mipakani hayana udhibiti wa kutosha, hivyo kusababisha waingie bila kudaiwa pasi za kusafiria.
Tunasisitiza kwamba kutembea na kitambulisho kunamfanya mtu aepukane na usumbufu na vilevile ni rahisi kwake kupata msaada kwa mtu au mamlaka yoyote, hivyo wote tujenge utamaduni wa kutembea na vitambulisho