Saturday, 3 September 2016

NSSF kujenga kiwanda kipya cha sukari Moro


KATIKA kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kutaka mifuko ya hifadhi ya jamii kuwekeza kwenye viwanda, Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), linashirikiana na ule wa Pensheni PPF kujenga kiwanda cha sukari kitakachozalisha tani 200,000 kwa mwaka.




Akizungumza na Nipashe katika mahojiano maalum juzi, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kayarara alisema kiwanda hicho kitajengwa katika eneo la Mkulazi lililopo mkoani Morogoro.
Profesa Kayarara alisema ekari 63,000 zimetengwa katika eneo la Mkulazi lililoko katika wilaya ya Morogoro.
Alisema mchakato wa ujenzi wa kiwanda hicho ulishaanza na wanategemea kazi itakamilika katika kipindi cha miaka miwili au mitatu toka sasa.

“Mradi huu ni ubia kati ya NSSF na Mfuko wa Pensheni PPF ila tungependa serikali iwepo ili Watanzania waone wana hisa pia,” alisema Profesa Kahyarara, ambaye aliteuliwa kuongoza NSSF, Machi 19, mwaka huu.
Profesa Kayarara alisema shughuli za kiwanda hicho zinatazamiwa kutoa ajira 100,000.
“Pia tumepanga kuwa na kilimo cha umwagiliaji ili kutoa nafasi kwa wakulima wa nje kulima miwa na kuuzia kiwanda,” alieleza Profesa Kahyarara.

Uendeshaji
Alisema uendeshaji wa kiwanda hicho utafanywa na wataalamu ambao watakuwa chini ya wanahisa.
Profesa Kahyarara alitolea mfano wa uendeshaji wa Benki ya Azania inayomilikiwa mifuko ya hifadhi ya jamii.

“Tutahakikisha kiwanda kinakwenda vizuri kwa kuwa tutaweka jicho letu. Tutaleta watendaji ambao ni wataalamu wa ngazi ya kimataifa ambao wakifanya vibaya watachukuliwa hatua,” alisema Profesa Kahyarara.
Profesa Kahyarara alisema kuwa wako kwenye hatua za mwisho za matayarisho ya barabara kuchongwa na kuwekwa kwa miundombinu ya umwagiliaji wa kisasa.
“Tutatumia teknolojia ya umwagiliaji wa kisasa wa matone. Na pia shamba lipo karibu na reli ya Tazara, itakuwa rahisi kusafirisha sukari hata nje ya nchi,” alisema.
MAHITAJI YA SUKARI NCHINI
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mahitaji ya sasa ya sukari ni tani 420,000.
Hata hivyo, takwimu za Bodi ya Sukari Tanzania zinaonyesha mahitaji ya nchi ni tani 320,000, huku viwanda vya ndani vya TPC, Mtibwa, Kagera na Kilombero vikizalisha tani 220,000 na kusababisha upungufu wa tani 100,000.
UCHUMI WA VIWANDA
Profesa Kahyarara alisema Tanzania imeamka na isipoweza kuwa nchi ya viwanda sasa, haitaweza tena.

“Tusikate tamaa na Rais watu asiachiwe mwenyewe, ametoa wazo watu walifuate na vitu vingi vinawezekana na siyo vigumu kama watu wanavyochukulia kwa kuwa hakuna biashara isiyo na matatizo,” alisema Profesa Kahyarara.
Mkurugenzi huyo alisema NSSF imejipanga kuingia kwenye uwekezaji wa viwanda na kwamba watakuwa makini kwa kuhakikisha wanachokifanya kinaingiza faida.
“Tunamshukuru Rais kwa kuona umuhimu wa kuwekeza kwenye viwanda, nchi haiwezi kuendelea bila kuwekeza kwenye viwanda, nchi zote zilizoendelea ziliwekeza huko,” alisema.
Pamoja na kiwanda cha sukari, Profesa Kahyarara alisema NSSF itajikita kwenye uwekezaji wa viwanda baada ya kufanya uchunguzi wa masoko, faida na hasara, baada ya uwekezaji kwenye majengo kutokuwa na faida kubwa.
Alitaja viwanda watakavyoanza navyo ni cha Viuadudu mkoani Pwani ambacho wametoa mkopo wa Sh. bilioni nne hivi karibuni, kinu cha kusaga unga mjini Iringa na kiwanda cha mafuta ya alizeti huko Dodoma.
“Kwa mfano wakulima wa mahindi Iringa tutawaingiza NSSF, mtu akipeleka magunia 10 ya mahindi basi gunia moja au nusu gunia itakuwa mchango wa NSSF, na wakulima wa alizeti pia itakuwa hivyo,” alifafanua.
Profesa Kahyarara alisema Tanzania imekuwa soko la bidhaa na mazao ya nje licha ya kupatikana kwa wingi nchini kwa kutolea mfano maziwa kutoka Dubai, Falme za Kiarabu (UAE) licha ya kuwapo ng’ombe nchini.
Alisema pia nguo zinaingizwa kwa wingi kutoka nje pamoja na kuwa Tanzania ni nchi ya tano kwa kulima pamba kwa wingi duniani.
Profesa Kahyarara alitaja pia korosho huku kukiwa na kilimo cha zao hilo katika mikoa ya Kusini.
“Hizo zabibu zinazouzwa Dar es Salaam na maeneo mengine nchini zinatoka Afrika Kusini wakati kuna zabibu zinalimwa kwa wingi Dodoma,” aliongeza Profesa Kahyarara.

CHANZO CHA VIWANDA KUFA
Mkurugenzi huyo wa NSSF alisema kwenye miaka ya mwanzo baada ya uhuru mwaka 1961, Tanzania ilipiga hatua kubwa ya ujenzi wa uchumi wa viwanda chini ya mpango wa maendeleo wa mwaka 1969 hadi 1974.
Alisema pia kulikuwapo mpango wa viwanda wa mwaka 1964 na mpango wa viwanda vya msingi ulioanzishwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Kwa mujibu wa Profesa Kahyarara miaka ya 70, Tanzania ilijitosheleza kwa kila kitu kuanzia vifaa vya shule kama madaftari, kalamu, karatasi na vifaa vya ujenzi huku akitaja baadhi ya viwanda kama kile cha mabati cha Aluminium Africa na kiwanda cha Saruji cha Wazo Hill.
Profesa Kahyarara alitaja viwanda vikubwa vya nguo 10 vilivyokuwapo enzi hizo kuwa ni Urafiki, Sungura, Kiltex, Ubungo Spinning, Mutex, Mwatex na Tabora Textile.
Tulikosea wapi?
Alipoulizwa sababu za Tanzania kurudi nyuma na kutegemea uagizwaji wa bidhaa za nje, alisema ni kutokana na mtikisiko wa uchumi duniani na nchi za Ulaya kuleta masharti kwa nchi zinazoendelea.
“Wenzetu walituwahi na kutudanganya ni sawa na mganga wa kienyeji anakwambia unaumwa kwa sababu umelogwa na mkeo, ndicho kilichoikuta Tanzania mwaka 1972 kwa kuwa kulikuwa na kupanda kwa bei ya mafuta iliyopanda kwa asilimia 400 katika soko la dunia pia kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), serikali kutumia fedha nyingi kununua ndege za kuanzisha Shirika la Ndege (ATC) na vita ya Kagera,” alibainisha.
Profesa Kahyarara alisema kutokana na hali hiyo serikali ilijikuta haina uwezo wa kuendesha viwanda kama kununua malighafi.

NIPASHE:

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!