RAIS John Magufuli amesema ndege ya kwanza kati ya nne zinazonunuliwa na serikali yake kwa ajili ya kufufua shirika la ATCL, itatua nchini Septemba 19 ikitokea Canada ilikotengenezwa.




Aidha, Rais alisema amebaini ufisadi wa Sh. bilioni 755 uliofanywa na wakandarasi katika upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza na ule wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Rais Magufuli aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akifungua mkutano wa 14 wa mwaka wa wahandisi uliohudhuriwa pia na viongozi wa kiserikali.
Magufuli pia alisema licha ya watu kuziponda ndege mpya mbili ambazo serikali inatarajia kuzinunua, ni lazima zitanunuliwa na kwamba ya kwanza itawasili nchini Septemba 19.
“Kuna watu wameanza kuziponda ndege, lakini hawajui kitu," alisema Rais Magufuli. "Nyie wahandisi mnajua vizuri, asiye mhandisi hawezi kujua.
"Na ninawahakikishia ndege zitakuja na ya kwanza itaendeshwa kutoka Canada hadi Tanzania.”
Rais alisema katika ununuzi wa ndege kuna vitu muhimu vinavyopaswa kuangaliwa ambavyo ni pamoja na matumizi ya mafuta, viwanja vya kutua kwa ndege hiyo na gharama za ununuzi wake.
Alisema ndege hizo zitakuwa na uwezo wa kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kwa saa 1:35.
UFISADI
Kuhusu kuwapo kwa harufu ya ufisadi katika upanuzi wa viwanja vya ndege, Rais Magufuli alisema katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza sh. bilioni 105 zilitumika katika upanuzi wa nusu kilometa ya njia ya kurukia, huku upanuzi wa JNIA ukitumia Sh. bilioni 650.

Kutokana na harufu hiyo ya ufisadi, Rais aliziagiza mamlaka husika kuanza kuchukua hatua kwa wale waliohusika kwa kuwa kisasi cha fedha kilichotumika ni kikubwa kulinganisha na uhalisia wa kazi.
“Nataka tufanye uchunguzi vizuri, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano upo hapa, haiwezekani pesa zote hizo zitumike katika kupanua sehemu ya uwanja, gharama hizo ni kubwa sana,” alisema Maguguli.
Alisema waliohusika na ubadhirifu huo ni watu walioaminika na serikali, lakini wameamua kuiibia.
Akifafanua zaidi kuhusu ufisadi huo unaodhaniwa kufanyika katika miradi hiyo, Rais Magufuli alisema mkandarasi aliandika magari ya kubebea kokoto yaliyotumika ni 200,000 badala ya 200.