WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amewaomba viongozi wa dini kuisaidia serikali katika mapambano ya kuwafichua wauza madawa ya kulevya na majambazi.


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba.

 

Nchemba alitoa ombi hilo wakati akifungua mkutano mkuu na kongamano la viongozi na wajumbe wa jumuiya kuu ya kanisa la Baptist Tanzania (BCT) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) mjini hapa.
Alisema serikali peke yake haiwezi kuwabaini majambazi na wauza unga wote ili kumaliza tatizo hilo lakini kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali, zikiwamo za kidini watu hao wanaweza kugundulika mara moja.
Waziri huyo alisema kuwa serikali inawaamini viongozi wa madhehebu ya dini katika kufanikisha suala hilo kwa kuwa yanafanywa na waumini wao.
“Chonde chonde viongozi wangu wa dini, ninapiga magoti kwenu kuwaomba muisaidie serikali katika kutoa taarifa za majambazi na wauza unga," alisema Nchemba kwa sababu "nyinyi ni rahisi kuwatambua kwa kuwa miongoni mwao ni washirika wazuri kwenye nyumba za ibada.”
Hata hivyo, aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanahubiri neno la mungu ili watu waweze kuachana na matendo maovu.
Alisema wanapohubiri kwenye nyumba za ibada suala linalohusu dhambi, amani na upendo, wengi wanaweza kuwa na hofu ya Mungu na kutokana na hilo watenda maovu wanaweza kuacha na serikali ikatulia.
Katika mkutano huo, Nchemba alitoa mifuko 200 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya BCT mjini Dodoma na fedha taslim sh. milioni moja kwa ajili ya uendeshaji wa mkutano huo.
Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Baptist Tanzania, Arnold Manase, aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kukaa meza moja na kuondoa tofauti zao.
Alisema kamwe amani haiwezi kupatikana kama viongozi wa pande zinazovutana hawatakaa meza moja kufanya mazungumzo ambayo yanaweza kuzaa makubaliano.
"Amani ya nchi ni muhimu sana hivyo kuna kila sababu ya viongozi wa siasa kukaa meza moja kutafuta mwafaka huku kazi kubwa ya viongozi wa dini wakiwa wanafanya maombi kwa ajili ya amani ya nchi isitoweke," alisema Askofu huyo.