Sunday, 18 September 2016

Muhimbili wahaha mashine mpya MRI


HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH), iliyoko jijini Dar es Salaam, inahitaji mashine mpya ya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali ijulikanayo kama Magnetic Resonance Imaging (MRI), kwani iliyopo inasuasua kutokana na kuharibika mara kwa mara.




Mkuu wa Idara ya Masuala ya Mionzi wa hospitalini hapo, Dk. Flora Lwakatare, aliyasema hayo juzi jijini Dar es Salaam, wakati akizungumzia kurejea kwa huduma hiyo MNH baada ya kusitishwa kwa zaidi ya wiki tatu.
Alisema kukosekana kwa MRI kwa kipindi hicho kumesababisha wagonjwa zaidi ya 900 kukosa huduma hiyo na kulazimika kuitafuta hospitali nyingine binafsi.
“Wagonjwa waliokuwa na maradhi ya muda mrefu ilibidi wasubiri na walio na matatizo ya kawaida walikwenda katika hospitali nyingine binafsi. Muda wote tulikuwa tukisubiri kifaa kilichoagizwa Uholanzi kadhalika betrii 31 za mashine hii zikibalibadilishwa ,” alisema.
Dk. Lwakatare alisema mashine hiyo imetumika zaidi ya miaka saba hivyo imechoka ndiyo maana inaharibika mara kwa mara na kwamba inafanyiwa matengenezo mara mbili kila mwaka.
“Kitaalamu kunahitajika mashine mpya… hii hutumika kuwapima wagonjwa waliopewa rufani na kuhitaji uchunguzi zaidi wa vipimo kwenye uti wa mgongo pamoja na ubongo,” alisema.
Alikumbusha kuwa Agosti 24, mwaka huu MRI iliharibika kutokana na hitilafu ya umeme, hivyo mafundi wa kampuni ya Philips ambao ni watengenezaji kwa kushirikiana na wataalamu wengine walianza kuikarabati.
Akizungumzia gharama alisema wagonjwa wanaopewa rufani katika hospitali za umma na kuhitaji kipimo hicho hulipia Sh. 210,000, wanaotumia bima ya afya pamoja na mifuko ya kijamii hulipia Sh. 300,000 hadi 350,000 huku wagonjwa binafsi wakitozwa Sh. 450,000.
Daktari Bingwa wa Masuala ya Mionzi, Musa Ndukeki, aliwatoa hofu wagonjwa wanaodhani kuwa mashine hiyo inamionzi na kueleza kuwa, ina sumaku sio mionzi.
“Mashine hii haina mionzi, kama wengi wanavyodhani ila ina sumaku, hakuhitajiki mgonjwa kuwa na aina yeyote ya chuma katika mwili wake anapokuwa anapimwa na mashine hii,” alisema

NIPASHE.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!