WATU watatu wameuawa katika matukio mawili tofauti, ambapo wawili wameuawa kwa kuchomwa moto na wananchi na mmoja ameuawa kwa kuchinjwa.
Mauaji hayo yote yanayohusishwa na imani za kishirikina, yalifanywa na wananchi zaidi ya 300 waliojichukulia sheria mkononi. Yalitokea Septemba 3, mwaka huu saa 8 mchana katika kijiji cha Nkindu kata ya Mbutu wilaya ya Nzega mkoani Tabora.
Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Godfrey Ngupulla alisema katika tukio la kwanza, Ezekiel Lazima (37) mkazi wa kijiji cha Nkundu kata ya Mbutu wilayani Nzega alitoweka kijijini hapo zaidi ya siku 20.
Hivyo, wananchi waliamua kupiga yowe (kauli ya kuashiria hatari) na kuanza kumtafuta na baadaye alikutwa akiwa ameuawa kwa kuchinjwa. Katika tukio la pili, Kashindye Halawa (27) aliuawa kwa kuchomwa moto na wananchi hao baada ya kutuhumiwa kuwa ndiye aliyefanya mauaji ya Ezekiel.
Kama hiyo haitoshi, wananchi hao walimkamata mganga wa jadi, Punguja Igokoro (47) wakimtuhumu kuwa ndiye aliyesababisha Kashindye afanye mauaji ya Ezekiel, na kumuua kwa kumchoma moto.
Ngupulla alisema uongozi wa wilaya unasikitishwa na kitendo hicho cha wananchi kujichukulia sheria mkononi kwa kuua watu bila kufuata taratibu na sheria za nchi.
Alisisitiza wote waliofanya mauaji hayo, watafikishwa katika vyombo vya dola kujibu tuhuma zitakazowakabili. Kwamba jitihada za kuhakikisha wilaya ya Nzega inakuwa salama, zinaendelea kufanyika hasa kwa kuanza na kura za maoni kijiji kwa kijiji.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nkindu, Kevin Malala alisema wananchi walikuwa na hasira na wao kama viongozi, walishindwa kuwazuia, licha ya kuwaomba kutofanya mauaji hayo.
Alisema walitishwa kuwa wangeendelea kuwaomba wasiue, hata wao wangeuawa. Katibu Tarafa ya Bukene, Rosia Swai alisema matukio hayo mawili, aliyashuhudia kwa macho.
Hata hivyo, alisema alishindwa kuwaomba wananchi hao kutokana na kutishiwa kuuawa. Baadhi ya watumishi wa serikali wanaoishi vijijini wamekuwa na hofu kubwa dhidi ya maisha yao kutokana na wananchi kutofuata sheria na taratibu za nchi.
Mwalimu Sembeiwe Henagula wa Shule ya Msingi Nkindu, alisema mauaji hayo yamewapa hofu wafanyakazi wa serikali. Aliomba serikali ilifanyie kazi suala hilo ili amani irudi na wananchi watii sheria zilizowekwa na mamlaka husika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Hamis Suleiman alikiri kutokea kwa mauaji hayo. Alisema Jeshi la Polisi litahakikisha watu waliofanya unyama huo wanapatikana na kufikishwa kwenye vyombo vya dola.
No comments:
Post a Comment