Wednesday, 7 September 2016

Mke wa bilionea Msuya awageuzia polisi kibao

ANAYEDAIWA kuwa mke wa marehemu Bilionea Erasto Msuya, mshtakiwa Miriam Msuya na mwenzake, wamedai mahakamani kwamba waliteswa na polisi na kulazimishwa kukiri kuhusika na mauaji ya Aneth Msuya, dada wa bilionea huyo.


mke wa marehemu Bilionea Erasto Msuya.



Madai hayo yalitolewa jana mbele Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Margareth Benkika, walipounganishwa na kusomewa hati mpya ya mashtaka ya mauaji ya Aneth.
Wakili wa utetezi, Peter Kibatala, alidai kuwa baada ya kuzungumza na washtakiwa wote wawili, wamemweleza kwamba waliteswa sana baada ya kukamatwa na kulazimishwa kukiri tuhuma hizo.
“Maelezo waliyoandika washtakiwa wote yalikuwa ni kutokana na mateso na wana alama zote ikiwamo kuvimba miguu na wana majeraha sehemu mbalimbali za miili yao,” alidai.
“Mheshimiwa naiomba mahakama kuliamuru Jeshi la Magereza nchini pale ambapo washtakiwa watakwenda mahabusu wafanyiwe uchunguzi wa kiafya kutokana na majeraha waliyoyapata wakiwa Polisi na majibu ya uchunguzi wa afya za washtakiwa hao yawasilishwe mahakamani kwa ajili ya kumbukumbu za kesi ili tuweze kuyatumia baadaye,” alidai Kibatala.
Akifafanua hoja zaidi, Kibatala alidai kuwa hati ya mashtaka ina upungufu kisheria kwa kushindwa kuonyesha nia ovu ya kutenda kosa hilo dhidi ya washtakiwa.
Upande wa Jamhuri uliomba muda wa kuwasilisha hoja za majibu ya utetezi kuhusu malalamiko yao.
Hakimu Bankika alisema kesi hiyo itatajwa Septemba 13, mwaka huu, na kwamba upande wa Jamhuri utawasilisha majibu kuhusu hoja za utetezi.
Mbali na Miriamu, mshtakiwa mwingine aliyeunganishwa katika kesi hiyo ni, mfanyabiashara Revocatus Muyela.
Lukondo, alidai Miriam (41) na Muyela (40), wote wafanyabiashara na wakazi wa Arusha, kwa pamoja wanakabiliwa na shitaka la mauaji ya Aneth, Mei 25, mwaka huu, maeneo ya Kibada, Kigamboni, Dar es Salaam.
Upande wa Jamhuri ulidaiwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Hata hivyo, mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwa mujibu wa sheria hadi upelelezi utakapokamilika kesi hiyo itahamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam

NIPASHE.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!