Thursday, 15 September 2016

Kizimbani kwa udhalilishaji mitandaoni


Dar es Salaam. Sheria ya mitandao imeendelea kung’ata, baada ya wakazi wa Dar es Salaam kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusomewa mashtaka tofauti ya kumdhalilisha Rais na Jeshi la Polisi kwenye mitandao.

Katika kesi ya kwanza, Dennis Temu (26), ambaye ni fundi magari anayeishi Tabata, alisomewa mashtaka ya kulidhalilisha Jeshi la Polisi kwenye mtandao wa WhatsApp.
Wakili wa Serikali, Salum Mohammed alidai mbele Hakimu Mkazi Mkuu, Emilius Mchauru kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Agosti 30, 2016 akiwa Tabata Bima, wilayani Ilala kwa kutumia mtandao wa WhatsApp kusambaza ujumbe usemao; “Nipo tayari kwa Ukuta naomba wanikabidhi askari 10 nipambane nao wakinishinda Mungu anihukumu. Tupigane mkono kwa mkono ‘pumbav’... zao”.
Temu amekana shtaka hilo na upande wa mashtaka ulidai upelelezi haujakamilika.
Mshtakiwa aliachiwa kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti ya kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao walisaini dhamana ya Sh500,000. Kesi hiyo itatajwa tena Oktoba 12.
Katika kesi nyingine, Suleiman Nassoro (20), fundi umeme anayeishi Kigogo Mbuyuni, amesomewa mashtaka ya kulidhalilisha Jeshi la Polisi kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kuandika ujumbe usemao; “safi sana aisee, mi naona wangekufa kama 20 hivi. Halafu Simon Sirro tumuulize mazoezi wanafanyia wake zao au” ambao aliutuma Agosti 25.
Lakini Nassoro amekana kutenda kosa hilo na upande wa mashtaka ulisema haujakamilisha upelelezi, jambo lililofanya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 27 itakapotajwa tena.
Mwingine ni dereva Juma Mtatuu (19) anayedaiwa kulidhalilisha Jeshi la Polisi kwa kutumia WhatsApp kwa kuandika; “huyu hata akifa ataenda peponi na kufanya mazoezi kote kule wamekufa Mbagala. Mimi nitakuwa wa kwanza kuandamana kule Kahama. Tarehe 1 Naelekea Kahama kwa Ukuta mimi nitakuwa namba moja kushika bendera ya Ukuta. Kifo kipo tu, usiogope kwani mawe na mapanga yameisha?”
Pia, mkazi wa Tegeta kwa Ndevu, Shakira Abdallah Makame amefikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na shtaka la kulidhalilisha Jeshi la Polisi kwa kutumia WhatsApp.
Katika ujumbe wake, Shakira anadaiwa kusema; “wakati tunajiandaa na Ukuta, wao wanajiandaa na ujambazi safi sana majambazi”.
Denis Wilson Mtegwa (27), alikuwa mmoja waliopandishwa kizimbani na kushtakiwa kwa kumdhalilisha Rais John Magufuli katika ujumbe wa WhatsApp alioutuma Agosti 24 akiwa Ubungo External wilayani Ubungo.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Kisutu, Dk Yohana Yongolo, ujumbe usemao; “JPM sijui anawaza nini kichwani, hata samahani hajui au nilikosea hajui. Nchi imefika hapa kwa sababu ya mtu mmoja aliyeamua kujilipua ufahamu wake.

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!