TATIZO la nyumba za walimu linatarajiwa kuwa historia, baada ya serikali kutenga Sh. bilioni 25 katika mwaka wa fedha wa 2016/17.




Hayo yalielezwa jana bungeni na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Bukene (CCM), Selemani Zedi.
Zedi alitaka kujua serikali haioni kuwa kuna umuhimu serikali kuu sasa ijenge nyumba za walimu wa shule za msingi vijijini hasa ikizingatia kuwa vijijini hakuna nyumba ambayo mwalimu anaweza kupanga.
Akijibu swali hilo, Jafo alisema serikali imetenga Sh. bilioni 13.9 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 1,157 kwa shule za msingi na Sh. bilioni 11.1 zimetengwa kujenga nyumba 661 kwa shule za asekondari nchini.
Aidha alisema kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari awamu ya pili (MMES II), serikali imepanga kujenga nyumba 183 katika shule za sekondari kwenye halmashauri mbalimbali zenye uwezo wa kuchukua familia sita kwa kila nyumba.
Hata hivyo alisema Halmashauri ya Wilaya ya Nzega katika mwaka wa fedha 2016/17 imetengewa sh. milioni 486.3 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu kwa shule za msingi na sekondari.