Thursday, 18 August 2016

Wanaosafirisha holela wasichana nje wakamatwe


KATIKA miaka ya karibuni kumekuwa na wimbi la baadhi ya Watanzania, kuwachukua Watanzania kwenda kuwatafutia kazi nje ya nchi.


Lakini, kampuni ambazo zimekuwa zikiwachukua watu hao kwa ajili ya kuwatafutia kazi hizo nje ya nchi, zimekuwa zikikiuka mikataba yao na kuwalazimisha kufanya kazi tofauti, ikiwemo ukahaba.
Kutokana na hali hiyo, tunaunga mkono kauli iliyotolewa hivi karibuni na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mindi Kasiga, kwamba serikali haitavumilia tena vitendo hivyo. Mindi alifafanua kuwa serikali itawarudisha nchini Watanzania 500 waliokwama India, baada ya kampuni zilizowapeleka huko, kukwama kuwatafutia kazi.
Kati ya Machi hadi Mei mwaka huu, balozi za Tanzania katika nchi za India na Malaysia, zilipokea maombi ya kusaidia kuwarejesha nyumbani Watanzania, ambao walipelekwa nchini India na Thailand kwa ahadi za kupatiwa ajira, zilizotolewa na watu wasio waaminifu, ambao wanashukiwa kujihusisha na mtandao wa biashara ya kusafirisha binadamu.
Mtandao huo mchafu huwa unawatafuta wasichana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 24 na hata chini ya umri huo, kwa kuwalaghai kuwa kuna fursa za ajira katika mahoteli, migahawa, maduka makubwa au kazi za nyumbani nchi za nje. Mtandao huo huwawezesha kwa kuwapatia hati za kusafiria na tiketi ya ndege, kwa ajili ya kusafiri kwenda nchi husika.
Wengi huvutika kirahisi kwa kuona hiyo ni fursa ya kujipatia kipato, lakini ukweli ni kwamba wengi hujua mapema kuhusu kazi wanayoenda kuifanya, huko ila ugumu wa maisha ndiyo unaofanya warubuniwe na kuingia kwenye matatizo makubwa.
Mindi alisema kwa India peke yake, kuna Watanzania takribani 500, ambapo New Delhi wapo 350, Bangalore 45, Mumbai 20 na wengine wengi wapo Goa. Kwa upande wa Mashariki ya Kati, wimbi kubwa la wasichana hurubuniwa kutafutiwa fursa, ikiwemo kazi za ndani, katika nchi za Oman, Saudi Arabia na Falme za Kiarabu.
Baadhi ya waathirika wamekuwa wakikimbilia kwenye ofisi za ubalozi, kuomba msaada. Tunapongeza ofisi zetu za Ubalozi, ambazo zimekuwa zikiwahifadhi ubalozini, kisha kuwasiliana na jamaa zao ili wawatumie nauli na kurejea nyumbani.
Kwa mfano, hivi karibuni katika Ubalozi wa Tanzania uliopo Oman, kulikuwa na wasichana 18 , ambapo 10 tayari wamesaidiwa kurudi na kuunganishwa na familia zao. Katika Ubalozi wa India, wasichana 15 wamepeleka maombi yao.
Tumebaini yapo matatizo mengi, yanayowakabili Watanzania hao katika nchi hizo za Mashariki ya Kati na Asia na baadhi yake ni kulazimishwa kufanya ukahaba na kunyang’anywa hati za kusafiria ili kuwadhibiti wasitoroke. Wengine hufanya ukahaba ili kurejesha gharama za kuwasafirisha pamoja na kupata nauli.
Matatizo mengine ni kufanya kazi bila mikataba, kufanya kazi nyingi ambazo zingetakiwa kufanywa na zaidi ya watu wawili au watatu, kufanya kazi kwenye familia zaidi ya moja tofauti na makubaliano, kufanya kazi bila muda maalumu wa kupumzika, kubaguliwa, kupigwa, kutopewa fursa ya kuwasiliana na mtu yeyote na kunyanyaswa kijinsia.
Tunaiomba serikali iwatafute wahusika wote wa mtandao huo wa kusafirisha binadamu hapa nchini na kuwakamata haraka kisha kuwafikisha mahakamani. Pia, serikali iendelee kufanya mawasiliano na serikali za nchi hizo, kukamata wahusika wa mtandao huo na kuwafikisha katika mkono wa sheria.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!