Rais wa chama cha Wakunga Tanzania (TAMA) bi.Feddy Mwanga akizungumza leo na waandishi.picha:maktaba

 

Mwenyekiti wa chama hicho, Rabisante Sama, alisema vifo vya uzazi vya mama na mtoto havitapungua endapo hakuna vituo vya afya vya kutosha.
Alisema pamoja na jitihada za serikali za kuweka nguvu zake katika kuimarisha huduma hiyo, lakini bado wanawake waliopo vijijini hawapati huduma ya uzazi inayostahili wakati wa kujifungua.
“Sisi tumekuwa tukifanya kazi nyingi sehemu mbalimbali mijini na vijijini, lakini huduma wanayopata wajawazito wa mijini, ni tofauti na wanayopata wa vijijini,” alisema.
“Vijiji vingi havina vituo vya afya kwa hiyo wajawazito wanalazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma na wengine hujifungulia majumbani kutokana na kushindwa kujiandaa mapema kwa safari ya kuifuata huduma hiyo,” aliongeza.
Sama alisema ili kuokoa vifo vya mama na mtoto, zipo hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa mapema ikiwa ni pamoja na kufanyiwa uchunguzi na kupewa rufani ya mapema mjamzito baada ya kubainika kuwapo kwa tatizo la uzazi.
Alisema kaulimbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni ‘Uchunguzi makini wa mjamzito na rufani ya mapema hupunguza vifo vya mama na mtoto mchanga.'
Alisema ipo haja ya mjamzito kuhakikisha anapata vipimo baada ya kujigundua kuwa na hali hiyo ili kuepusha matatizo yanayoweza kujitokeza baadaye.
Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Muhammed Bakari, alisema tatizo ambalo bado wanakabiliana nalo kwa sasa katika utoaji wa huduma ya afya ya uzazi, ni wauguzi na wakunga wengi kukosa lugha nzuri wanapowahudumia wagonjwa.
“Nimesikia changamoto zenu na tutazifanyia kazi, lakini niseme kwamba bado tuna tatizo la wauguzi na wakunga wengi wenye midomo michafu kwa wagonjwa, wengi hawatoi maneno mazuri wakati wanawahudumia wagonjwa, ninaaomba chama chenu kifanye kazi hiyo ya kuwaelimisha kuondokana na tabia hiyo,” alisema Profesa Bakari.