Rais wa Simba, Evans Aveva.
TAASISI ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) inawashikilia Rais wa Simba, Evans Aveva na wajumbe wengine wote wa kamati yake ya utendaji isipokuwa wawili, kwa tuhuma za kuchepusha fedha za klabu hiyo kinyume cha taratibu.
Taarifa zaidi ambazo gazeti hili lilizipata kutoka ndani ya uongozi wa Simba, zilieleza kuwa hadi kufikia jana jioni, wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji ya Simba, walikuwa wamefikishwa kwenye ofisi za Takukuru kwa ajili ya kuhojiwa isipokuwa Zacharia Hanspope na Ally Suru.
Aveva alihojiwa na taasisi hiyo kwa zaidi ya saa 10 jana akituhumiwa kuhamisha fedha za ada ya uhamisho wa mchezaji Emmanuel Okwi kutoka kwenye akaunti ya Simba na kujiwekea kwenye akaunti yake binafsi.
Hivi karibuni, Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) liliitaka klabu ya Etoile Sportive du Sahel (ESS) kuilipa Simba fedha za mauzo ya mchezaji huyo dola za Marekani 300,000 (sawa na Sh. milioni 645) baada ya awali klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Tunisia kupuuza kulipa ada ya uhamisho huo uliofanyika Januari 2014.
Ofisa Habari wa Takukuru, Tunu Mleli, aliiambia Nipashe jana kuwa wanamshikilia Aveva kwa makosa ya uchepushaji wa fedha.
Hata hivyo, habari za ndani ambazo gazeti hili lilizipata jana jioni zilieleza kuwa Takukuru itaendelea kumshikilia kiongozi huyo wa klabu ya Simba hadi pale itakapowahoji watu wengine ambao ameshirikiana nao.
"Huyu kupata dhamana kwa leo bado haijafahamika maana wanatafutwa alioshirikiana nao katika kosa hilo ili upelelezi ukamilike,” kilieleza chanzo chetu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime, alithibitisha kukamatwa kwa Aveva huku akieleza kuwa walimhifadhi kwenye kituo cha polisi cha Urafiki.
Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi usiku na watu wa Takukuru na kumfikisha kituoni hapo kwa ajili ya kusubiri mahojiano na maofisa wa taasisi hiyo nyeti.
Habari za ndani kutoka kwenye kituo hicho cha polisi zilieleza kuwa Aveva alifikishwa saa mbili usiku akiwa amefungwa pingu.
“Hapa tulimpokea kwa ajili ya kumhifadhi, Takukuru walikuja asubuhi kumchukua, huyo Rais ni mtu maarufu sana ila kwenye uongozi wa Rais John Magufuli, hakuna cha mtu maarufu, ukilamba cha mtu lazima ukione, huwezi amini kaletwa usiku akiwa kafungwa pingu,” alisema mtoa habari wetu.
Chanzo chetu kilieleza kuwa Hanspope ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba yuko nje ya nchi wakati Suru alikuwa hajakamatwa bado na maofisa wa Takukuru.
No comments:
Post a Comment