MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesema kuwa itaanza msako wa nyumba kwa nyumba kuhakiki gharama za upangishaji ili kutoza kodi ifikapo Septemba mwaka huu.





Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo, aliiambia Nipashe wiki hii iliyotaka kufahamu utekelezaji wa suala hilo.
Alisema huo ni utekelezaji na mikakati ya TRA katika kuongeza makusanyo ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 na kwamba, yeyote atakayejaribu kukwamisha ikiwa ni pamoja na wapangaji kutoa taarifa potofu, watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Wiki iliyopita TRA, ilisema mkakati mwingine ni kusajili walipakodi wapya na kuhuisha taarifa zao katika namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN).
"TRA imepanga kufikia lengo lililopo na kulivuka, aidha TIN ambazo hazitumiki zitafutwa na tutapita nyumba kwa nyumba kuhakiki gharama za upangishaji ili kukokotoa kodi sahihi ambayo ilikuwa hailipwi serikalini," alisema Kayombo.
Aidha, taarifa ya makusanyo ya kodi ya Julai mwaka huu, ambayo ni Sh. trilioni 1.055, sawa na asilimia 95.6 mapato hayo ni ya kwanza kwa mwaka mpya wa fedha wa 2016/2017.
Makusanyo hayo yanatajwa kupanda ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana, wakati mapato yalipokuwa Sh. bilioni 914, hivyo ongezeko hilo kuwa asilimia 15.43.
TRA, mwaka huu wa fedha, imepanga kukusanya Sh. trilioni 15.1 ikilinganishwa na lengo la Sh. trilioni 13.32 la mwaka wa fedha 2015/16.
Aidha, mamlaka hiyo ilisisitiza wateja wanaonunua bidhaa kuhakikisha wanachukua risiti na kwamba ambao watakamatwa na wakaguzi wakiwa hawana risiti, watapewa adhabu ya kutodai risiti ambayo ni faini ya kati ya Sh. 30,000 hadi Sh. 1,500,000, kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015.
Kayombo alisema mamlaka inaendelea kuhuisha taarifa za walipakodi ikiwamo kupiga picha, kuchukua alama za vidole na vielelezo muhimu vya mlipakodi ili kuhakikisha kila mfanyabiashara na biashara inakuwa na TIN moja.

NIPASHE.