SERIKALI imepiga marufuku uingizwaji wa makaa ya mawe na jasi (Gypsum) kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuendeleza viwanda vya ndani na kujitegemea.
Akizungumza na wadau na wazalishaji wa madini ya makaa ya mawe na jasi, jana Dar es Salaam, Naibu Waziri, Wizara ya Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani alisema wawekezaji watakaokiuka amri hiyo kuanzia sasa, makaa au jasi itazuiliwa ili isiingizwe nchini.
Alisema uzalishaji wa makaa ya mawe umefikia tani milioni tano ambayo hayajachimbwa na kwamba viwanda vinatumia tani 50 na mahitaji yaliyopo ni tani 37,000. Pia alisema madini ya jasi yapo tani 354,000 na watumiaji waliopo ni 30,000 hivyo viwanda vinahitaji uzalishaji wa madini hayo.
Alisisitiza watazungumza na Kituo cha Uwekezaji (TIC) kuhakikisha hakuna wawekezaji wa ndani watakaoagiza makaa ya mawe au jasi nje ya nchi.
Aidha, alisema kuwa wazalishaji na wanunuzi wa madini hayo, wanatakiwa kuingia mikataba rasmi ambayo pia watazungumzia kuhusu bei ya kununulia na gharama za uzalishaji.
No comments:
Post a Comment