Saturday 6 August 2016

Serikali yakata rufaa sheria ya ndoa

SERIKALI imeamua kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu uliosema kipengele cha umri wa mtoto wa kike kuolewa chini ya miaka 18 kwamba kinakiuka Katiba kwa nia ya kuufanya uamuzi huo kuwa sheria.


Uamuzi wa Mahakama Kuu uliitaka Serikali kufuta vifungu viwili cha 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 vinavyoeleza mtoto wa miaka 14 na 15 anaweza kuolewa kwa idhini ya mzazi au Mahakama.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe alisema kuwa Serikali imeamua kukata rufaa Mahakama ya Rufani dhidi ya uamuzi huo si kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, bali kupata uamuzi wa chombo cha juu cha Mahakama ambao hautaweza kubadilishwa na hivyo kuwa kama sheria.
Aliyasema hayo jana Dar es Salaam alipokutana na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) ambao walimtembelea ofisini kwake kuzungumzia mambo kadhaa likiwemo suala hilo la serikali kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.
Dk Mwakyembe alisema si kwamba serikali inapingana na uamuzi wa Mahakama Kuu ila kinachofanyika ni utaratibu wa kawaida ambao utaiwezesha Serikali kuwa na uamuzi kutoka katika chombo cha juu kabisa cha Mahakama nchini.
Alisema uamuzi huo hautaweza kutenguliwa na mtu au chombo chochote na kuongeza kuwa ukibaki uamuzi huo pekee katika ngazi hiyo ya Mahakama inaweza ikatokea siku nyingine Jaji mwingine akatoa uamuzi tofauti na huo.
Awali, Taasisi ya Msichana Initiative ilifungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu ya Tanzania, shauri namba 5 la mwaka 2016 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikihoji uhalali wa kikatiba wa kifungu cha 13 na 17 cha Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 unaoidhinisha mtoto wa kike wa miaka 14 na 15, kuolewa kwa idhini ya mzazi au Mahakama.
Mahakama Kuu iliamuru vifungu hivyo vifutwe kwa kuwa viko kinyume cha Katiba ambayo inatamka kuwa umri wa mtoto ni hadi miaka 18 na kuolewa katika umri huo ni kuvunja sheria mama (Katiba).

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!