Friday, 19 August 2016

Mifuko ya plastiki mwisho mwaka huu

SERIKALI imepiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki nchini kuanzia Januari mosi, mwakani.



Hatua hiyo imelenga kuepuka athari za kiafya na kimazingira zitokanazo na mifuko hiyo.
Kutokana na agizo hilo, kuanzia mwaka mpya, ni marufuku kuagiza, kuzalisha, kuuza na kutumia mifuko hiyo ya kwenye vifungashio vya maji na bidhaa nyingine.



Aidha, serikali imezitaka wizara, mamlaka, mashirika, idara, viwanda, Jeshi la Polisi na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc), kuhakikisha uzalishaji na matumizi ya mifuko hiyo yanakoma siku ya mwisho ya mwaka huu.
Katika tangazo lililotolewa jana kwenye baadhi ya magazeti na Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, ilielezwa kuwa serikali imetoa muda uliobaki wa miezi minne ili wamiliki wa viwanda vyote vya kuzalisha mifuko ya plastiki kuchukua hatua kwa kuwekeza katika mifuko mbadala na kutumia mfumo wa urejeshaji taka za plastiki.
Tangazo hilo lilieleza kuwa matumizi ya mifuko hiyo yanaathiri afya za watumiaji pamoja na mazingira kutokana na mifuko hiyo kuzagaa, kutooza na kuathiri udongo, kuziba mifereji na kusababisha mafuriko.
Pia lilieleza kuwa mifuko hiyo inaharibu mfumo wa ikolojia na bionuwai na inasababisha vifo kwa wanyama wanapoimeza huku afya za binadamu zikiwa hatarini kutokana na baadhi yao kuitumia kufungashia vyakula vya moto.
"Mifuko hiyo inaharibu hewa kutokana na watu wengi majumbani kuitumia kwa ajili ya kuwashia mkaa kwa matumizi ya kupikia," ilisomeka sehemu ya tangazo hilo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!