Sunday, 7 August 2016

Miaka 36 bila medali ya Olimpik

 

NI miaka 36 imepita sasa tangu Tanzania ilipotwaa medali kwa mara ya kwanza na mwisho katika Michezo ya Olimpiki iliyofanyika Moscow, Urusi mwaka 1980. Wanariadha Filbert Bayi na Suleiman Nyambui ndio walioitoa kimasomaso Tanzania baada ya kutwaa medali za fedha katika mbio za meta 3,000 kuruka gogo na maji na meta 5,000.


Hakuna ubishi kuwa hao ndio hadi sasa `vidume' wa Michezo ya Olimpiki kwa upande wa michezo yote, ambayo Tanzania imekuwa ikipeleka wachezaji katika michezo hiyo inayofanyika kila baada ya miaka minne.
Michezo ya mwaka huu Michezo ya mwaka huu ni ya 31 tangu kuanza kufanyika na wenyeji ni Rio de Janeiro, Brazil na Tanzania imepeleka wachezaji saba tu kutoka katika michezo mitatu.
Michezo hiyo ni riadha, ambayo ina wachezaji wanne wa marathon, ambao ni Alphonce Felix, Said Makula, Fabian Joseph na mdada pekee katika riadha, Sarah Ramadhani. Waogeleaji ni pamoja na Magdalena Moshi na Hilal Hemed Hilal, ambao watashiriki katika mchezo wa meta 50 mtindo huru huku judo wakipeleka mchezaji mmoja tu, Andrew Thomas.
Makocha wa timu hizo ni Francis John (riadha), wakati yule wa kuogelea ni Alexander Mwaipasi, huku wa judo ni Hamisi Zaidi na daktari wa timu hiyo ya Tanzania ni Nassoro Matuzya.
Michezo hiyo inafanyika kwa mara ya kwanza kabisa katika nchi ya Amerika ya Kusini, hivyo yanatarajia kuwa ya aina yake.
Nafasi ya upendeleo Ukiondoa wachezaji watatu wa riadha, Joseph, Felix na Makula, wachezaji wengine wote waliobaki wamefuzu kwa kupitia nafasi ya upendeleo. Wachezaji hao waliofuzu kwa upendeleo huwa na nafasi ndogo sana ya kufuzu kupata medali kwani huwa na mlolongo mrefu sana kwa mchezaji kupata medali.
Nafasi ya upendeleo imekuwa ikitolewa baada ya nchi husika kuomba na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) iliweka nafasi hiyo ili kuziwezesha nchi zote kushiriki michezo hiyo hata kama haina mchezaji aliyefuzu. Na ndio maana lengo kubwa la Michezo ya Olimpiki ni kushiriki na suala la medali linakuja baada ya ushiriki wa timu.
Hata timu hiyo ya Tanzania ina nafasi kubwa ya kushiriki na sio kushindana, kwani maandalizi ya timu zetu hayakuwa mazuri licha ya makocha wa timu hizo kutoa ahadi kibao wakati wa kuagwa kwa timu hiyo.
Kila mchezo katika michezo hiyo ya Rio 2016 ya Olimpiki na Paralympic imewekewa vigezo, ambapo wachezaji na timu wanatakiwa kuvifikia ili kufuzu kushiriki michezo hiyo.
Medali katika Olimpiki Bayi na Nyambui walirudi nyumbani na medali za fedha kutoka katika Michezo ya Olimpiki ya Moscow ya mwaka 1980 baada ya kushika nafasi ya pili katika mbio za meta 3,000 kuruka gogo na maji na meta 5,000.
Bayi pia ndiye aliyeweka rekodi za dunia za mbio za meta 1,500 katika Michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika Christchurch, New Zealand mwaka 1974 baada ya kuwashinda John Walker na Ben Jipcho.
Kwa mara ya kwanza Tanzania ilishiriki Michezo ya Olimpiki mwaka 1964, ambapo ilichukua miaka takribani 16 kutwaa medali katika michezo hiyo. Sasa ni miaka 36 hakuna medali yoyote. Katika michezo ya mwaka huu ya Rio, ni jambo gumu sana kwa Tanzania kurejea rekodi ya mwaka 1980 kwa kurudi na medali kutoka katika michezo hiyo, kwani maandalizi hayakuwa ya kutosha.
Tayari Mkuu wa msafara wa timu, Jabir Suleiman alikaririwa na vyombo akisema kuwa sio rahisi kurudi na medali, hivyo alishauri maandalizi ya Olimpiki ya mwaka 2020 Tokyo, Japan yaanze mara baada ya michezo ya Rio.
Alisema kuwa wenzetu wamekuwa wakianza mapema maandalizi, hivyo vyama vya michezo nchini vijitahidi kufuata nyayo za wengine ili kusaka mafanikio hayo.
Joseph alikaririwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akisema ni ndoto kwa Tanzania kupata medali kutoka katika michezo hiyo. Alisema maandalizi yalikuwa yakisuasua na kambini hawakuwa hata na daktari, hivyo matibabu yalikuwa magumu kwao.
Hata hivyo, mwanariadha huyo wakati wa kuaga timu ya Olimpiki alisema wamejiandaa vizuri, lakini huenda alisema hivyo kutokana na shinikizo kutoka kwa viongozi wa Riadha Tanzania (RT) na wengine.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!