Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema hakuna mtu mwenye hatimiliki ya nchi, hivyo kuzuiwa vyama vya siasa kufanya siasa hadi mwaka 2020 si sahihi.
Akizungumza jana katika mahojiano na kipindi cha Funguka kinachorushwa na Azam Tv, Lowassa ambaye alikuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu uliopita kupitia Chadema akiungwa mkono na Ukawa alisema kazi ya vyama vya siasa ni kuwafikia wananchi mahali popote walipo.
“Kama Rais anakwenda Kahama, kwa nini mimi nizuiwe kwenda Mbeya na Iringa kukutana na wananchi?” Alihoji Lowassa ambaye sasa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na kusisitiza: “Amri amri hizi hazitasaidia, ni lazima tukae na kuzungumza. Hakuna mtu mwenye hatimiliki ya nchi hii.”
Akiwa mkoani Singida juzi, Rais John Magufuli alisema viongozi wa vyama vya siasa watatakiwa kufanya mikutano ya kisiasa kwenye majimbo waliyochaguliwa tu na si vinginevyo kauli.
Rais pia amekuwa akisisitiza kwamba siasa za ushindani majukwaani ziachwe hadi 2020 na sasa wananchi waachwe wafanye kazi.
Serikali kuhamia Dodoma
Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu Serikali kuhamia Dodoma, Lowassa alisema: “Ni uamuzi mzuri lakini wasiende kwa kasi wasije wakavunjika miguu.”
Alisema Dodoma ni mahali pazuri pa kuhamia lakini wasichukue fedha za miradi ya maendeleo kwa ajili ya posho za kuhamia Dodoma.
Alisema viongozi wa awamu zote walikuwa na dhamira ya kuhamia Dodoma.
“Rais wa Awamu ya Kwanza, Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete wote walikuwa na dhamira ya kuhamia Dodoma, tatizo lilikuwa vipaumbele vya wakati ule,” alisema.
Kususia Bunge
Alipoulizwa kuhusu wabunge wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia Bunge linapoongozwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, Lowassa alisema uamuzi wao ulikuwa mzuri kwa sababu hawakufurahishwa na uamuzi wa kiongozi huyo.
Alisema tatizo hilo lilitokea kwa sababu Spika wa Bunge, Job Ndugai alikuwa na matatizo ya kiafya lakini kama angekuwapo lisingetokea.
Alisema wabunge kutoka nje ya Bunge ilikuwa njia ya kuonyesha kutoridhishwa na uamuzi wa Naibu Spika.
“Nina uhakika Spika wa Bunge, Job Ndugai ni makini na kama angekuwapo tatizo hilo lisingetokea kwa sababu ya busara zake katika uendeshaji wa Bunge,” alisema.
Hata hivyo, alisema Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/17 imepita bila wabunge wa vyama vya upinzani kuwapo, jambo ambalo si zuri kwa demokrasia nchini.
Utendaji wa Rais Magufuli
Kuhusu utendaji wa Rais Magufuli, Lowassa alisema anafanya kazi nzuri hasa katika sekta ya elimu, lakini yeye angefanya tofauti.
Alisema katika elimu kama angekuwa rais, angeanza kutatua matatizo ya walimu na kuboresha masilahi yao badala ya madawati.
Alisema walimu wana matatizo ya muda mrefu ambayo yamekuwa yakirudisha nyuma maendeleo ya elimunchini.
“Ni kweli anafanya kazi nzuri lakini tatizo la madawati ni eneo dogo katika elimu, angeangalia pia masilahi ya walimu kwani matatizo yao yana mchango mkubwa katika kudorora kwa elimu hapa nchini,” alisema.
Alisema jambo jingine ni tatizo la ajira. Alisema hilo lingekuwa la msingi kuanza kushughulikia.
Hata Rais wa Marekani, Barack Obama amezungumzia suala la ajira na akaeleza kwamba ametengeneza ajira za kudumu milioni 1.5 tangu aingie madarakani.
“Kwa hiyo kusema hivyo sina maana Rais Magufuli hafanyi kazi, bali anafanya kazi nzuri,” alisema.
Hajutii kuhama CCM
Alipoulizwa kama hajutii kuhama CCM, Lowassa alisema hajutii na akaeleza kwamba uamuzi wake ulikuwa sahihi kutokana na mambo yaliyofanyika.
Alisema alihama chama hicho baada ya kutungwa tuhuma dhidi yake lakini hakupewa nafasi ya kujitetea.
“Tuhuma zilitungwa, huko nyuma chama chetu kilikuwa na utaratibu wa kuitwa na kuhojiwa kuhusu tuhuma zinazokukabili, lakini hawakufanya hivyo. Walijua nina watu wengi wanaoniunga mkono, ndiyo maana hawakunipa nafasi ya kujieleza.”
Alisema walifanya hivyo kwa kuwa walikuwa na mtu wao waliyekuwa wakitaka apitishwe kugombea urais.
“Kwa bahati nzuri mtu wao naye hakufanikiwa kupitishwa kugombea nafasi ya urais kupitia CCM,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu urafiki wake na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete na taarifa kwamba alishiriki kuondoa jina lake katika vikao vya juu vya CCM, Lowassa alijibu: “Wacha watu wengine wamhukumu na yeye mwenyewe ajihukumu.”
Alipoulizwa kuhusu urafiki wake na Kikwete kama bado unaendelea, Lowassa alisema, “Sijamwona hivi karibuni lakini sina mgogoro naye.”
Kashfa ya Richmond
Lowassa aliyejiuzulu uwaziri mkuu kutokana na kashfa ya mitambo ya kufua umeme ya Richmond, alisema hakuna mtu asiyejua suala hilo hivyo asingependa kulifafanua kwani limedumu kwa zaidi ya miaka 10 akisema limeandikiwa mpaka vitabu na baadhi wamepata vyeo kwa suala hilo, hivyo watu wote wanalifahamu.
Kuimbwa NEC ya CCM
Alipoulizwa kuhusu namna alivyojisikia watu walipokuwa wakiimba wimbo wa kumshabikia kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) mwaka jana, Lowassa alisema ulikuwa ni uamuzi wao na wala hakuwa anaelewa kama tukio hilo lingetokea.
“Sikujisikia chochote kutokana na hali ilivyokuwa, lakini nadhani ulikuwa uamuzi wao, siwezi kusema kama walikuwa sahihi au hawakuwa sahihi ila walieleza walichokuwa wakikitaka,” alisema
Mipango yake 2020
Akizungumzia alivyojipanga, Lowassa alisema kukiwa na Katiba nzuri na tume ya huru uchaguzi, ana uhakika mwaka 2020 ataingia Ikulu.
“Tumemaliza uchaguzi ingawa haukuwa huru na haki. Lakini haina maana kuuzungumzia hivi sasa na kuumizana mioyo, suala la msingi ni kujipanga kwa ajili ya mwaka 2020,” alisema.
Zanzibar
Kuhusu Zanzibar, Lowassa alimtaka Rais Magufuli asipuuze malalamiko yanayotolewa na wananchi wa Zanzibar.
“Wananchi wanalalamika kwamba wanapigwa na vyombo vya dola, tusiwapuuze ni lazima tuangalie namna ya kuwasaidia,” alisema.
Alisema kama kulikuwa na mazungumzo yaliyozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, katika utawala wa Rais Aman Karume na kukawa amani, “Kwa nini Magufuli asisimamie mazungumzo ili kuleta SUK na kuleta amani hivi sasa?”
No comments:
Post a Comment