“KIAFYA, hakuna faida yoyote ya kukeketa mwanamke, badala yake kuna madhara makubwa. Miongoni mwa madhara hayo ni kipindi cha kujifungua, kwani mwanamke anapokeketwa kovu linapona lakini wakati wa kujifungua kovu hilo halina uwezo wa kutanuka, hivyo mama anachanika sana na kupoteza damu nyingi.”
Maneno hayo anayasema Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akinamama katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Januarius Hinju wakati wa mdahalo ulioandaliwa na Mtandao wa Kimataifa wa kupinga ukeketaji na ndoa za utotoni uitwao Youth For Change Tanzania chini ya Shirika la Global Citizen na kufanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Dk Hinju anaongeza: “Halikadhalika, hata watoto wanaozaliwa na wanawake waliokeketwa baadhi wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na mama kuwa na uchungu mkali kwa muda mrefu na kuna hatari pia ya mtoto kufia tumboni.” Anasema kimsingi, vitendo vya ukeketaji vimekuwa vikichangia vifo vya akinamama wakati wa kujifungua ambapo wakati mwingine njia ya uzazi hupasuka na kuungana na njia ya haja kubwa.
Anasema bado suala la ukeketaji limeendelea kujichimbia katika jamii nyingi kutokana na kuhusishwa au kuingizwa kwenye imani za kimila. Anabainisha kuwa asilimia 26 ya wanawake wanaojifungua katika hospitali ya mkoa wa Dodoma wamekeketwa na kwamba takwimu za mwaka 2013 zinaonesha kwamba kati ya wanawake 11,226 waliofika hospitalini hapo kujifungua wanawake 1,966 walikuwa wamekeketwa ambao ni sawa asilimia 28.
Aidha anasema mwaka uliofuata, yaani 2014, jumla ya akinamama 13,195 waliojifungua, kati yao 1,436 walikuwa wamekeketwa. Ni kutokana na tatizo la ukeketaji kundelea kujichimbia katika jamii hata katika karne hii, Dk Hinju anasema kuna haja ya kufanyika kwa utafiti nchi nzima ili kuona ukubwa wa tatizo la ukeketaji. Hata hivyo, anasema takwimu za hospitali yao zinaonesha idadi ya wanawake waliokeketwa wanaofika kujfungua imekuwa ikipungua lakini si kwa kasi walioitazamia.
Meneja wa Miradi na Ujengaji Uwezo wa Amref Health Africa Tanzania, Dk Pius Chaya anashauri kuwe na mipango ya kuwezesha mabaraza ya wazee wa kimila ili yawe sehemu ya kutoa elimu juu ya masuala ya ukeketaji na ndoa katika umri mdogo. Akizungumza katika mdahalo huo, Dk Chaya anasema mabaraza ya wazee yakiwezeshwa yanaweza kuwa chachu ya mabadiliko na hivyo kupunguza vitendo vya ukeketaji ambavyo vinaonekana kushamiri baadhi ya maeneo.
Anasema katika baadhi ya maeneo wazee wa kimila wamekuwa wakipata mgao kutokana na fedha zinazopatikana kwa kuwafanyia wasichana ukeketaji hivyo ni muhimu wakaelimishwa madhara na hivyo kuwa sehemu ya kutoa elimu. “Mangariba wamekuwa wakipata fedha nyingi mpaka milioni kadhaa kwa mwaka na asilimia 20 ya fedha zinakwenda kwa viongozi wa kimila. Kwa mtindo huo suala la ukeketaji haliwezi kuisha,” anasema.
Dk Chaya anaamini kwamba wazee wengi wa kimila hawajapata elimu ya kutosha kuhusu madhara ya ukeketaji na ndoa za utotoni, hali ambayo imekuwa ikichangia kuendelea kwa vitendo hivyo. Anasema kuna mafunzo ya kuwaandaa watoto wa kike (unyago) kuishi kwenye ndoa. Anasema hayo ni mambo yenye faida lakini kwa bahati mbaya katika jamii zinazokeketa mafunzo hayo huingiziwa dhana potofu za ukeketaji kama suala la muhimu pia katika ndoa.
Pia anasema suala la kutoa elimu lisiangalie tu kwenye kukeketa bali na wale waliokeketwa na kupata matatizo kama ugonjwa wa fistula. Naye anawataka vijana wasomi kufanya tafiti ili kuwe na uhakika wa takwimu zinazotolewa kuhusiana na vitendo hivyo. Kwa upande wake, Dk Philemon Sengati anataka nguvu kubwa ielekezwe katika kutoa elimu ili kubadilisha mitazamo ya watu.
“Suala la elimu kila moja anafahamu ni msingi wa ufanisi na maendeleo ya suala lolote katika dunia hii kwani unapoongelea elimu unampatia mtu maarifa na kuongeza ujuzi katika jamii zilizostarabika,” anasema. Anasema wasomi wana nafasi kubwa ya kusaidia kumaliza tatizo la ukeketaji na ndoa za utotoni kwani mtu aliyesoma anaheshimika katika jamii. “Unapokuwa na elimu unaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kufanya mabadiliko na kupambana na masuala ambayo ni hasi katika jamii yako,” anasema.
Mwanachama wa Youth for Change, Naamala Brighton naye anasema elimu ni njia pekee itakayosaidia jamii kuachana na vitendo vya ukeketaji na ndoa za utotoni. “Elimu ni kifutio maana inafuta ujinga wote na kuwa na mtazamo tofauti. Bila elimu vitendo hivyo havitakwisha,” anasema. Emmanuel Mang’ana kutoka Shirika la Plan International anasema vijana ni chachu kubwa ya mabadiliko na wana nafasi kubwa katika kuelimisha jamii juu ya madhara ya kiafya dhidi ya vitendo hivyo.
Anasema katika mikoa ya Lindi na Mtwara ndoa zimekuwa kikwazo kikubwa kwa maisha ya wasichana kwani kilo tano tu za sukari zinaweza kufanya mzazi amuozeshe binti yake. “Machi mwaka huu nilikuwa katika wilaya ya Simanjiro, cha kushangaza wanaume wa Kimasai walisema hawaoni kama kuna shida katika suala la kukeketa watoto wa kile lakini hilo linatokana na mitazamo potofu waliyonayo,” anasema.
Mang’ana anasema miaka ya nyuma hata ndoa za utotoni zilikuwa ni nyingi lakini vyombo vya habari vimesaidia sana katika kuhabarisha wananchi na kuibua madhara yake. Ni kwa msingi huo anapongeza serikali kupeleka umeme vijijini, hali ambayo imesaidia sana watu kupata habari kupitia redio na luninga na hivyo anahimiza serikali kuzidi kupeleka umeme zaidi katika vijiji ambavyo bado havijapata.
Mwanachama mwingine wa Youth For Change, Upendo Abisai anasema utamaduni wa kukeketa wasichana ni utamaduni uliodumu katika jamii kwa muda mrefu na kwamba kuondoa imani hiyo kunahitaji kuwa na imani nyingine ambayo itapatikana kwa elimu itakayobadilisha mitazamo ya watu. “Elimu ni njia pekee itakayosaidia kuwabadilisha watu mitazamo,” anasema.
Anasema elimu inaweza kutolewa kwa njia mbalimbali na vijana wasomi wanaweza kuisaidia jamii kwa kuishawishi na hivyo kubadilisha mtazamo wao kuhusu mila na desturi zilizopitwa na wakati. Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema ukeketaji kwa watoto na wanawake ni janga la kitaifa kutokana na kuwa na athari nyingi.
Kumekuwa na idadi kubwa ya watoto wanaofanyiwa vitendo hivyo ambapo takwimu zinaonesha kuwa katika mkoa ya Manyara kila watoto 100, 71 wamekeketwa, Dodoma kwa kila watoto 100, watoto 64 wamekeketwa, Arusha kwa kila watoto 100, watoto 59 wamekeketwa, mkoani Singida kila watoto 100, watoto 51 wamekeketwa na mkoani Mara kila watoto 100, watoto 40 wamekeketwa.
Waziri huyo anasema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 15 ya wanawake (karibu wanawake na wasichana milioni 7.9) hapa nchini wamekeketwa. Anasema ukubwa wa tatizo la ukeketaji katika mikoa hiyo linatokana na imani potofu na dhana hiyo imeanza kujitokeza katika mikoa mingine kama Dar es Salaam, Morogoro na Pwani kutokana na watu wa makabila mbalimbali kuhamia mikoa hiyo.
“Serikali inapinga, inalaani na kukemea tabia ya kuendelezwa kwa vitendo hivi vya ukatili unaodhalilisha mtoto wa kike na mwanamke kwani unamsababishia madhara makubwa kiafya, kielimu, kisaikolojia na kimaendeleo. “Ndani ya serikali ya Rais John Magufuli tutamaliza vitendo vya ukeketaji lazima tuseme basi kwenye ukeketaji,” anasema. Anasema serikali itaendelea kutekeleza programu mbalimbali za hamasa na elimu kwa jamii zinazojikita katika kubadili fikra na mitazamo ya wananchi dhidi ya ukeketaji.
Takwimu zilizokadiriwa kuwa wanawake na wasichana milioni 7.9 nchini Tanzania wamefanyiwa ukeketaji. Ripoti ya afya na utafiti wa kaya ya Tanzania inakadiriwa ukeketaji kwa wasichana na wanawake wa kati ya miaka 15 hadi 49 ni asilimia 14.6 kwa mwaka na hiyo imepungua kidogo kwa asilimia 17.9 mwaka 1996. Ukeketaji unatajwa kuwa na athari nyingi kwani wengine hufariki kutokana na kupoteza damu nyingi au kwa ugonjwa wa kuambukizwa. Pia waliokeketwa wanaweza kupata matatizo wakati wa uzazi.
No comments:
Post a Comment