Wednesday 3 August 2016

Chadema yakomalia Ukuta





CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kinakinaendelea na maandalizi ya uzinduzi wa operesheni ya Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta), ambayo itakwenda sambamba na uzinduzi wa mikutano ya hadhara nchi nzima, itakayoanza Septemba Mosi, mwaka huu.




Sambamba na kusisitiza hilo, imesema inamshangaa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kwa kuunga mkono kauli ya Rais John Magufuli kwamba hakuna mikutano ya kisiasa kwa kuwa uchaguzi ulishamalizika.
Naibu Katibu Mkuu Chadema, Salum Mwalimu, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari.
Alisema operesheni hiyo imelenga kupaza sauti za Watanzania ambao wanaumizwa na msimamo wa serikali ya awamu ya tano kutokana na kauli ya Rais Magufuli kwamba wakati wa siasa umekwisha hadi mwaka 2020 kwa kuwa kinachotakiwa hivi sasa ni utekelezaji wa ahadi za serikali kwa Watazania.
Mwalimu alisema kauli hiyo ya Rais, ambayo iliungwa mkono na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, ililenga kuminya demokrasia na kuvunja katiba ya nchi.
"Msajili wa vyama, Jaji Mutungi ni mwanasheria ambaye anafahamu sheria. Alipoiunga mkono kauli ya Rais kwamba shughuli za kisiasa hadi mwaka 2020, yeye kama mlezi wa vyama nchini, hakutenda haki na anafahamu kuwa hilo halitekelezeki. Tutafanya mikutano ya hadhara nchi nzima kupitia Ukuta," alisema Mwalimu.
Alisema tayari operesheni hiyo imeungwa mkono na wadau mbalimbali, wakiwamo wanasheria, wafanyabiashara, mama lishe na baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mwanzoni mwa wiki hii, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, alisema Kamati Kuu imejadili kwa kina hali ya kisiasa nchini na kutoa maazimio ya kutekeleza operesheni hiyo.
Mbowe alisema tangu kuanza kwa utawala wa awamu ya tano, matukio ya kuminya demokrasia na kwenda kinyume cha utawala bora yameshaumiza Watanzania, huku wengi wao wakikosa sehemu ya kusemea.
Alisema suala la kujenga Ukuta halitachagua itikadi za chama wala dini na kwamba kila mpenda haki na demokrasia ya kisiasa ana haki ya kushiriki katika operesheni hiyo

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!