Tuesday 5 July 2016

WATU BINAFSI MARUFUKU KUSAFIRISHA BINADAMU

JESHI la Polisi nchini limesema lina mpango wa kufuta utaratibu wa usafirishaji wa watu nje ya nchi, unaofanywa na watu binafsi.


Limesema kazi hiyo sasa itaachiwa kampuni zinazotambulika, zitakazokuwa chini ya wizara inayohusika na masuala ya kazi. Limebainisha kuwa tatizo la biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu ndani na nje ya nchi ni kubwa; na kwamba zinahitajika jitihada mahsusi kwa kushirikiana na wananchi katika kukabiliana nalo.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam juzi na mpelelezi anayeshughulikia makosa dhidi ya usafirishaji wa binadamu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mrakibu wa Polisi, Lucy Ngonyani. Alisema hayo katika semina ya waandishi wa habari juu ya kupambana na kuzuia biashara hiyo haramu, iliyoandaliwa na Shirika la Msaada wa Kisheria (NOLA).
Akiwasilisha mada ya ‘Hali halisi ya biashara hiyo nchini’, Ngonyani alisema kitengo chake, kimekuwa kikipokea matukio mengi ya usafirishwaji haramu wa binadamu, unaohusisha raia wa Tanzania na nje.
“Hali ni mbaya kutokana na ukweli kuwa wengi wa waathirika wanaosafirishwa tumegundua kuwa hutumikishwa katika kazi za ngono, kazi ngumu na wakati mwingine huchukuliwa viungo vyao,” alisema Ngonyani.
Alisema pamoja na kuwepo kwa biashara ya kusafirisha binadamu nje ya nchi na kutumikishwa kingono na kazi ngumu, pia nchini kumekuwepo na tatizo sugu la kuwatumikisha wafanyakazi wa ndani walio chini ya umri unaoruhusiwa kufanya kazi.
Alisema kazi ya udhibiti wa biashara hiyo, imekuwa ni ngumu kutokana na uelewa mdogo wa waathirika, ambao kutokana na hali duni ya maisha, hurubuniwa kuwa huko waendako kuna ajira nzuri zitakazowaongezea kipato.
“Ndio maana tumeanzisha operesheni katika ofisi za Uhamiaji, tumeweka kitengo cha kudhibiti usafirishaji huu haramu, msichana tunayedhania kuwa anaweza kuathirika aliyekuja kuomba hati ya kusafiria huwa tunamuhoji kwanza mpaka tutakapojiridhisha ndio tunamruhusu,” alisisitiza.
Alisema kupitia operesheni hiyo, mwaka 2014 pekee walibaini wasichana waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu 20 kwa siku na kufanikiwa kuwaokoa.
Aidha, alisema wamewatia hatiani washtakiwa watatu akiwemo raia wa India, Mtanzania na Mkenya na kuokoa wasichana kadhaa wa Nepal, Burundi na Tanzania, waliosafirishwa na kutumika kwa ajili ya ngono bila ridhaa yao.
“Pamoja na raia huyu wa India aliyewatumikisha wasichana raia wa Nepal kazi ya ngono badala ya kutumbuiza ngoma yao ya asili, pia tumewakamata wanawake wawili mmoja Mtanzania na mwingine Mkenya waliokutwa na wasichana wa Kinondoni waliokuwa wanapelekwa Kenya kwa ajili ya biashara ya ukahaba,” alisema.
Aliiomba jamii vyombo vya habari, kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwafichua wahusika wa biashara hiyo haramu, inayowatumbukiza katika adha ya maisha waathirika wengi. “Hasa vyombo vya habari tunaomba muielimishe jamii kuhusu ukubwa wa tatizo hili. Wengi hudhani kwamba kwenda nje ya nchi ndio ‘dili’ wakati si kweli,” alieleza.
Katibu wa Sekretarieti ya Kamati ya Kitaifa ya Kuzuia Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Biadamu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Seperatus Fella alisema kwa hali ilivyo, Tanzania ni chanzo, mkondo na nchi kusudio la safari kwa waathirika wanaolazimishwa kufanyakazi ngumu na biashara ya ngono.
“Kasi ya matukio ya usafirishwaji haramu wa binadamu Tanzania inazidi kasi ya biashara hiyo ya kimataifa na mbaya zaidi hurahisishwa na ndugu, marafiki au madalali baada ya kupewa ahadi ya elimu, au ajira yenye faida mijini au nje ya nchi,” alisisitiza Fella.
Wakili wa Kujitegemea kutoka NOLA, Dotto Joseph alisema shirika hilo kwa kushirikiana na mashirika mengine matatu, walianzisha mradi wa kuweka mifumo ya ulinzi na rufaa kwa watoto dhidi ya biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu, unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU).
Mashirika hayo mengine ni International Organization for Migration (IOM), Faraja Vocational Training Centre (Faraja) na Young Domestic Workers Organization.
Alisema lengo la mradi huo ni kuanzisha mifumo thabiti ya ulinzi kwa waathirika wa biashara hiyo, ambao wengi ni wanawake na watoto na kuwezesha upatikanaji wa takwimu sahihi za matukio ya biashara hiyo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!