WAKATI serikali ikisema itaendelea kushirikiana na nchi ya Kongo katika nyanja mbalimbali zikiwamo za kidiplomasia, kibiashara, utalii, utamaduni na uchumi ili kuwaenzi waasisi wa nchi hizo, Watanzania wamekaribishwa katika nchi hiyo kuwekeza kwenye sekta ya madini, kilimo na nishati.
Balozi wa Kongo nchini, Mutamba Jean Pierre akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje,Balozi Dk.Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk.


Agustine Mahiga pamoja na Balozi wa Kongo nchini, Mutamba Jean Pierre, wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 56 ya Uhuru wa Kongo yaliyofanyika Ubalozi wa Kongo jijini Dar es Salaam.
Mahiga alisema urafiki wa Tanzania na Kongo ulianza miaka ya nyuma na kwamba uliunganishwa na marais wa nchi hizo ambao kwa sasa ni marehem, Mwalimu Julius Nyerere na Patrice Lumumba.
"Urafiki huu hauwezi kufa hata siku moja, tumekuwa tukishirikiana katika mambo mbalimbali kama vile bandari, kulinda amani na ujenzi wa miundombinu ikiwamo barabara na reli," alisema Balozi Mahiga.
Kwa upande wa Jean Pierre, alisema atadumisha uhusiano uliokuwapo kati ya Tanzania na Kongo kwa kuboresha utoaji na upatikanaji wa viza kirahisi.
"Wakati leo (jana) tunaadhimisha uhuru wa nchi yetu, sina budi kuwashukuru wale wote ambao mmekuwa mkishirikiana na kufanya kazi nasi, wakiwamo wafanyabiashara kutoka Kongo, marafiki na pia wawekezaji ambao wamekuwa wakifika hapa ubalozini wakihitaji kujua maeneo ya uwekezaji nchini Kongo," alisema Pierre.
Balozi Pierre alisema Watanzania wanakaribishwa Kongo kuwekeza katika maeneo ya utalii, kilimo, biashara, nishati na madini, miundombinu pamoja na maeneo mengine yenye manufaa.
Alisema alipokutana na Rais John Magufuli, aliambiwa kaulimbiu yake ni "Hapa Kazi Tu", na kwamba katika kumuunga mkono rais Magufuli na kauli yake hiyo, naye ameanzisha kaulimbiu isemayo "Hapa ni Kazi Sana".