Monday 18 July 2016

WANNE WABABMBWA NA MADAWA YA KULEVYA


JESHI la polisi mkoani hapa linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kukamatwa na madawa yadhaniwayo kuwa ni ya kulevya aina ya heroine, fedha pamoja na vifaa vya kuandaa madawa hayo zikiwemo Biblia tatu.



Kamanda wa polisi mkoani Morogoro, Ulrich Matei alisema jana kuwa watuhumiwa hao walikamatwa Julai 14, saa 10 jioni katika eneo la Chamwino manispaa ya Morogoro wakati jeshi hilo likiwa katika utekelezaji wa misako ya kudhibiti uhalifu inayoendelea mkoani hapa.
Kamanda Matei aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni pamoja na Halima Iddy (23) mkazi wa Darajani, Fikira Hussein (36) Shabani Mlonge (30) na Hamadi Issa (33) wote wakiwa ni wakazi wa Chamwino Manispaa ya Morogoro.
Kamanda huyo alisema watuhumiwa hao walikamatwa na madawa hayo ya kulevya ambayo yalishindwa kutambulika uzito wake huku yakiwa yamefungwa kwenye mfuko wa Nailoni na mengine yakiwa kwenye kete 16 pamoja na vifaa vya kuandaa madawa hayo.
Alivitaja vifaa hivyo kuwa ni pamoja na Vioo 4, kipimo maalum cha kupimia uzito, biblia 3 ambazo hutumika kutoa karatasi nyepesi za vifungashio, simu 6 za aina mbalimbali ambazo wanunuzi huziweka rehani ili kupata madawa hayo, na pesa taslimu kiasi cha Shilingi mil 3,734,000 zinazosadikiwa kuwa ni za mauzo ya madawa hayo.
Wakati huo huo kamanda Matei alisema jeshi hilo linamshikilia mtu mmoja kwa tuhuma za kukamatwa na dola 76 za kimarekani ambazo ni bandia zikiwa za dola 100 kila moja.
Kamanda Matei alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika matukio tofauti ambapo katika tukio la kwanza Peter Mwakihonga (30) mkazi wa Malinyi alikamatwa akiwa na dola hizo bandia za kimarekani.
Kamanda huyo alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa na askari waliokuwa doria julai 13, saa 4 usiku katika eneo la misegese kata ya mwembeni tarafa ya Malinyi wilayani Malinyi.
Wakati huo huo Raia wa Burundi Ramadhani Saidi (50) Mtusi na mkazi wa Urambo mkoani Tabora anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani hapa baada ya kukamatwa akiwa na noti bandia za shilingi 10,000 zikiwa jumla nakala 1060 pamoja ambazo zingekuwa sawa na thamani ya shilingi mil 10,620,000.
Kamanda Matei alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Julai 14, saa 5 asubuhi katika eneo la Uhindini kata ya kasiki wilayani Kilosa mkoani hapa.
Kamanda huyo alisema kuwa mtuhumiwa huyo pia amekutwa akiwa na picha zenye michoro ya Shilingi 5000 na 10,000 pamoja na baadhi ya malighafi za kutengenezea noti hizo.
Hata hivyo kamanda huyo alisema mtuhumiwa huyo anaendelea kuhojiwa ili kubaini uhalali wa uraia wake ambapo atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika

NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!