Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi, Wilbroad Mutafungwa



WANAWAKE wawili wakazi wa Moshi, wamesherehekea vibaya sikukuu ya Eid el Fitr, baada ya kukamatwa kwa nguvu na kubakwa na vijana waliodai kuwatambua kwa sura, ambao kwa sasa wanatafutwa na polisi.





Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi, Wilbroad Mutafungwa, amethibitisha kutokea kwa matukio hayo kwa nyakati tofauti juzi, maeneo ya Kilacha na Mabogini, wilaya ya Moshi.
“Kuna baadhi ya matukio ya kutisha yanayohusu ukatili wa wanawake kubakwa yamejitokeza wakati wa sikukuu ya Eid el Fitri. Wahusika waliofanya ubakaji huo tunawatafuta ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema.
Kamanda Mutafungwa alisema tukio la kwanza lilitokea Kilacha, kata ya Makuyuni, Jimbo la Vunjo, ambapo mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 18 (jina limehifadhiwa), alifanyiwa ukatili huo Julai 6, mwaka huu, majira ya saa 4:00 usiku, akiwa anatokea njia panda ya Himo kuelekea nyumbani kwao Matala.
“Inadaiwa wakati akielekea Matala alitokea kijana mmoja ambaye hakufahamika jina na kumkamata kwa nguvu kisha kumwangushwa chini na kumbeba kichakani na kumbaka kisha kutokomea kusikojulikana,” alisema.
Alisema tukio la pili, mfanyabiashara na mkazi wa Uru Mamboleo mwenye umri wa miaka (24) naye alikamatwa kwa nguvu na kubakwa, akiwa njiani kuelekea nyumbani kwa baba yake anayeishi eneo la Mandaka Mnono, kata ya Mabogini.
Kamanda Mutafungwa alisema kabla ya kitendo hicho, mwanamke huyo (jina limehifadhiwa), alimuomba kijana mmoja aliyekutana naye amuelekeze barabara ya kwenda kwa baba yake na ndipo alimpomgeuka na kumvutia kichakani na kisha kumbaka.
Mbali na ukatili huo, kamanda huyo wa polisi mkoa wa Kilimanjaro alisema polisi mkazi wa Kiboriloni ambaye ni kondakta wa daladala kwa tuhuma ya kukutwa na kete nne za dawa za kulevya ambayo hadi sasa hazijafahamika ni aina gani.