Wednesday, 6 July 2016

Wanandoa, mtoto wafa wakitoka kwa wakwe

WANANDOA na mtoto wao walikuwa miongoni mwa watu 31 waliofariki kwenye ajali ya mabasi mawili ya kampuni ya City Boys yaliyogongana uso kwa uso juzi katika kijiji cha Maweni, wilaya ya Manyoni, mkoani Singida




baadhi ya wananchi wakiwa kwenye mstari nje ya chumba cha kuifadhia maiti katika hospitali ya rufani dodoma kutambua miili ya watu waliopoteza maisha kwenye ajali ya mabasi mawili ya kamapuni ya City boy.

Mabasi hayo yaliyokuwa yanatokea Kahama, mkoani Shinyanga, yaligongana majira ya saa 8.15 mchana juzi na kusababisha majeruhi 54.
Akizungumza na Nipashe jana kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, ndugu wa marehemu hao, Saidi Mussa alisema baba yake mdogo Peter Sinto (32), mkewe, Joyce William (26) na binti yao Neema Peter (2), walifariki kwenye ajali hiyo wakitokea Wilaya ya Urambo, mkoani Tabora kwenda Morogoro.
Mussa alisema Sinto ambaye alikuwa mwalimu kwenye Shule ya Sekondari ya Mvomero, mkoani Morogoro alikuwa anatokea Urambo ambako alikwenda kwa ajili ya utambulisho baada ya kufunga ndoa na mkewe Joyce miaka mitatu iliyopita katika Kanisa la Mashahidi wa Jehova, Mbarali, mkoani Mbeya.
Alisema Sinto alikuwa likizo, hivyo alitumia nafasi hiyo kwenda Urambo kwa ajili ya kumtambulisha mkewe kwenye familia yao.
“Alikwenda kutambulisha familia yake maana alifunga ndoa Mbeya ambako ni kwa upande wa mwanamke hivyo akaona atumie kipindi chake cha likizo kuitambulisha familia kwa ndugu zake Tabora pamoja na mtoto wao,” alieleza Mussa kwa masikitiko.
Mussa alisema alipata taarifa juu ya tukio hilo baada ya kupigiwa simu na mama yake na kujulishwa kuwa katika ajali hiyo alikuwamo Sinto na familia yake.
Alisema waliamua na mama yake kwenda mara moja kwenye Hospitali ya Rufani ya Dodoma ili kutambua miili.
“Sikuwasiliana na Peter wakati anasafiri ila nilijua suala hilo baada ya kutaarifiwa na mama juu ya ajali,” alisema Mussa wakati akimzungumzia Sinto ambaye alisomea Chuo Kikuu cha Dodoma.
Naye mtoto wa dada wa marehemu Sinto, Stephano Anthony, alisema marehemu watasafirishwa kwenda kuzikwa Urambo.
MDOGO WA MBUNGE AFARIKI AJALINI
Katika ajali hiyo pia taarifa zinaeleza kuwa, miongoni mwa waliofariki ni pamoja na mdogo wa Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, Ismail Bashe, aliyekuwa akitoka Dar es Salaam kuelekea Nzega, huku wadogo wake wengine wawili wakiwa majeruhi.

MAITI ZATAMBULIWA
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma, Dk. Ibenzi Ernest, alisema jana kuwa maiti za watu waliofariki 31 kwenye ajali hiyo zimeanza kutambuliwa.

Dk. Ibenzi alisema vifo viliongezeka na kufikia 31 kufuatia mmoja wa majeruhi aliyekuwa amelazwa wodi ya wagonjwa mahututi (ICU) kufariki dunia jana.
Alisema juzi walipokea maiti 27 na majeruhi 15 wa ajali hiyo. Majeruhi saba walitibiwa na kuruhusiwa na waliobaki nane walilazwa hospitalini hapo.
Dk. Ibenzi, hata hivyo, alisema miili 13 kati ya 28 imetambuliwa na ndugu wa marehemu hao na kuchukuliwa kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Alitaja miili iliyotambuliwa kuwa ni John Lukanda, Ismail Bashe, Paul Mfaume, Dicles Wajubigiri, Rabia Lema, Levoso Israel, Lesta Exavel, Kefin Deus, Pauline Meza, Deogratus Mamunyu, Betty Ancent, Jesca Lazaro na Leonard Chacha.
Alisema wagonjwa wawili waliolazwa ICU ni Katra Abubakari (12) na mwingine ambaye hajafahamika jina lake kutokana na kuumia kichwani na kukosa fahamu.

Majeruhi wengine ni Athuman George, Jamila Mathias, Mjaidi Waziri, Monica Laban na Disko Wabale.
Dk. Ibenzi alisema utambuzi wa marehemu hao ni mgumu kutokana na sura zao kuharibika vibaya, huku kukiwapo miili ambayo ilikuwa haina vichwa.

“Kuna mwili hapa umetambuliwa lakini kichwa hakikupatikana. Pia kuna viungo tu vya mwili vilivyoletwa hapa kwa mfano kuna ubongo wa mtu umeletwa hapa, vingine vipo pembeni sijajua ni vingapi mpaka ndugu waje kutambua ili viunganishwe na miili,”alisema mganga huyo.
Akizungumzia suala hilo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Dk. Francis Mwanisi, alisema hospitali yake juzi ilipokea majeruhi 54 wa ajali hiyo, lakini hadi kufikia jana alikuwa amebakia majeruhi mmoja pekee mwanamke.
“Leo (jana) tuliwapa rufani ya Dodoma wagonjwa watatu, 36 waliruhusiwa hivi sasa tumebakiwa na mgonjwa mmoja mwanamke,” alisema Dk. Mwanisi.
CHANZO CHA AJALI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka, aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa, uchunguzi wa awali wa jeshi hilo umebaini chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa madereva wote wawili.

“Hawa madereva walipofika eneo la kijiji cha Maweni, wote wawili walionyesha ishara ya kuwasiliana kwa kuwashiana taa na kila mmoja kuhama upande mmoja kwenda mwingine hali iliyopelekea washindwe kumudu magari hayo,” alisema Sedoyeka.
Kamanda Sedoyeka alisema tayari jeshi lake limemtia mbaroni dereva Jeremia Martine (34), mkazi wa Dar es Salaam aliyekuwa akiendesha basi namba T 247 BCD pia linamsaka Bonface Mwakalukwa wa basi lingine T 531 DCE (yote Scania), ambaye alitoroka baada ya ajali.
Ajali hiyo ilitokea kijiji cha Maweni, kata ya Mvumi, Tarafa ya Kintinku, wilaya ya Manyoni, mkoani Singida, mabasi hayo yalipokuwa yakipishana huku madereva wakifanya mzaha, lakini mmoja wao (aliyekuwa anatokea Kahama) kutokana na ugeni wake alishindwa kuielewa ishara hiyo.
KAMANDA MPINGA AZUNGUMZIA AJALI
Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga, wakati akitoa taarifa ya jeshi hilo kuhusu hali ya salama barabarani nchini, jijini Dar es Salaam jana, alisema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa imechangiwa na uzembe wa madereva na mwendokasi.

Alisema madereva wa mabasi hayo walitaka kusalimiana kwa kushikana mikono huku magari yao yakiwa katika mwendokasi.
Alisema madereva wa mabasi hayo walipokaribiana waliwashiana taa kisha wakasogeleana upande wa kulia kwa dhumuni la kusalimiana ndipo walipogongana.
Kamanda Mpinga alisema madereva wamekuwa wakikiuka kwa makusudi sheria inayowataka kuendesha kwa mwendo usiozidi kilometa 80 kwa saa na kwamba basi lililokuwa likitokea Kahama kwenda Dar es Salaam kabla ya kupata ajali lilikamatwa Singida mjini likiwa na mwendokasi wa kilometa 122 kwa saa na dereva kuandikiwa faini ya Sh. 30,000, lakini aliendelea kuendesha kwa uzembe hadi ajali ilipotokea.
Kadhalika, Kamanda Mpinga alisema katika kipindi cha wiki moja kuanzia Julai Mosi hadi nne, mwaka huu kumetokea ajali tatu ambazo zimesababisha vifo vya watu 46 na majeruhi 73.
Kamanda alitaja ajali hizo kuwa moja ilitokea eneo la Dakawa kwa malori mawili kugongana na kuwaka moto hivyo kusababisha vifo vya watu watano na kesho yake basi la kampuni ya Otta lilipata ajali eneo hilo na kusababisha vifo vya watu sita baada kugonga moja ya lori lililopata ajali.
MABASI 12 YA CITY BOY YAFUNGIWA
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), imeyafungia mabasi ya Kampuni ya City Boy kutoa huduma ya usafirishaji hadi hapo uchunguzi wa kina uliosababisha ajali hiyo utakapokamilika.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe, alisema katika uchunguzi wa awali wamebaini kwamba ajali hiyo ilisababishwa na uzembe na mwendo kasi na kwamba uchunguzi zaidi wa kubaini chanzo cha ajali hiyo umeanza kufanywa.
Alisema wamechukua hatua hiyo kupitia kifungu cha sheria ya Sumatra namba 9 ya mwaka 2000 ili kujiridhisha na sifa za madereva pamoja na viwango vya ubora wa magari yanayomilikiwa na kampuni hiyo.
Alisema jumla ya mabasi hayo yaliyosimamishwa ni 12 na kwamba ukaguzi utafanywa na mkaguzi wa magari kutoka Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani.
Mbali na mabasi ya kampuni hiyo, alitaja mengine yaliyofungiwa ni Mohamed Trans kutokana na makosa mbalimbali yakiwamo ya ubovu pamoja na utoaji mbovu wa huduma.
Kadhalika, alisema mabasi ya Otta Safari, ambayo yanafanya safari za masafa marefu yamefungiwa na kwamba yataruhusiwa kutoa huduma baada ya kufanyiwa uchunguzi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!