Friday 15 July 2016

Ufaransa wampongeza Magufuli kukabili ufisadi


UFARANSA kupitia ubalozi wake nchini, imempongeza Rais John Magufuli kwa kuhakikisha viashiria vya demokrasia vinaimarishwa kwa lengo la kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi wake.


Taifa hilo ambalo jana liliadhimisha Siku ya kitaifa ya Ufaransa, maarufu kama Bastille Day, limesema vita ya Magufuli dhidi ya ufisadi na kutowajibika kwa utumishi wa umma ni moja ya uimarishaji wa demokrasia nchini.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Balozi wa Ufaransa nchini Melika Berak amesema kwamba taifa lake linatambua juhudi anazofanya Rais Magufuli katika kuhakikisha usalama waTanzania na maendeleo.
Alisema juhudi za kuimarishwa taasisi za demokrasia kunakofanywa na rais Magufuli kunachochea maendeleo na uadilifu katika utumishi wa umma. Akizungumzia mahusiano duniani, alisema dunia inahitaji ushirikiano mkubwa wa kikanda kama inataka kujiimarisha na kuwa na maendeleo yanayokidhi mahitaji ya binadamu leo na kesho.
Aliisihi Tanzania kuendelea kuwapo katika jumuiya za kikanda kwa lengo la kukabiliana na uchumi kubwa ambazo bila wao kushirikiana kikanda hawawezi kupata ushindani unaotakiwa.
Akihutubia kwa lugha ya kifaransa huku akichanganya na Kiingereza kwa wageni waalikwa mbalimbali wakiwemo mawaziri, mabalozi wa nchi mbalimbali na wananchi wa kawaida makao makuu ya ubalozi huo jijini Dar es Salaam, Balozi Berak alisema taifa lake litaendelea kuchangia maendeleo ya Tanzania.
Alisema kwa mwaka jana ubalozi wake ulisaidia kufanikisha midahalo ya wazi inayogusa mazingira na mabaliliko ya tabia nchi, makongamano ya kiuchumi na ushirikiano wa tasnia ya sanaa na kusema kwamba mwaka huu itaimarisha maeneo hayo.
Katika sherehe hizo ambapo watu mbalimbali mashuhuri walikuwapo akiwamo Waziri Mkuu mstaafu Salim Ahmed Salim, Waziri wa Madini na Nishati, Profesa Sospeter Muhongo, Mwenyekiti Tume ya haki za binadamu, Serikali iliwasilishwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Suzan Kolimba.
Naibu waziri ambaye alimwakilisha Waziri wake Dk Augustine Mahiga, aliipongeza Ufaransa kwa siku yake hiyo ya kitaifa na kuahidi ushirikiano wa Tanzania na Ufaransa kukuzwa zaidi.
Aidha, alishukuru misaada ya Ufaransa kwa Tanzania hasa katika sekta ya miundombinu, kilimo na maji na kuitaka jamii ya Tanzania kutumia ushirikiano uliopo wa kiserikali kutanua wigo katika uwekezaji.
Aliitaka jamii ya Watanzania kutumia jukwaa lililopo la ushirikiano kati ya Tanzania na Ufaransa katika biashara na viwanda kupata mapatna ambaowatashirikiana nao kufanikisha taifa hili kuwa la uchumi wa viwanda kwa kutumia rasilimali zilizopo hapa nchini. Katika historia, Bastille ni ngome ya zamani ambayo ni gereza iliyopo mjini Paris.
Watu wengi wa Ufaransa wanahusisha ngome hii na utawala wa kikatili wa falme ya Bourbon katika miaka ya mwishoni ya 1700. Julai 14, 1789, vikosi vilivyoasi vilivamia Bastille ukawa ndio mwanzo wa mapinduzi ya Ufaransa, na Julai 14, 1790 kukawepo na makubaliano yaliyowezesha kuanzishwa kwa utawala wa kifalme wa kikatiba.
Mwanasiasa Benjamin Raspail ndiye aliyependekeza Julai 14 kuwa mapumziko nchini Ufaransa, sheria ilipitishwa Julai 6,1880 na kuanzia Julai 14 Bastille Day ikawa siku ya mapumziko.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!