MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania imesema uchunguzi wa kitaalamu bado unaendelea ili kubaini iwapo bawa la ndege lililookotwa na wavuvi katika Kisiwa cha Kojani Pemba ni mabaki ya ndege ya Malyasia .
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo Vallery Luanda Chamlungu ameyabainisha hayo wakati wa makabidhiano ya bawa hilo yaliyofanyika katika bandari ya Kojani na kushuhudiwa na Viongozi wa mbali mbali wa Serikali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Wete .
Alisema , pamoja na uchunguzi wa kitaalamu unaofanywa na mamlaka hiyo , lakini pia Uongozi unaendelea kuwasiliana na mashirika ya ndege ya kimataifa ya ili kusaidia kukamilisha machakato wa kutambua asili ya ndege hiyo .
“Uchunguzi bado unaendelea ili kubaini kwamba bawa hilo ni mabaki ya ndege ya Malyasia iliyopotea miaka kadhaa iliyopita , tunafanya mawasiliano na mashirika ya ndege ya kimataifa na hili bawa tunatarajia wenzetu kutoka Malyasia watakuja ”alifahamisha Chamlungu .
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo alisema wataendelea kushirikiana na wananchi kufanya utafiti hasa sehemu za baharini sambamba na kuwashukuru wavuvi wa Kojani kwa kuweza kulihifadhi bawa hilo .
Aidha , Mkuu wa Wilaya ya Wete Rashid Hadid Rashid akikabidhi bawa hilo aliwataka wananchi kuwasiliana na vyombo vya ulinzi wanapookota vitu baharini , na kuacha kuvihifadhi majumbani kwani baadhi vinaweza kuwa ni hatari kwa maisha yao .
Alisema , Serikali ya Wilaya ilisimamia ili kuona kwamba bawa hilo linahifadhiwa , na linabaki katika mazingira yaliyo salama ili kupisha uchunguzi wa kitaalam ufanyike .
“Pamoja na juhudi zenu , lakini pia naomba nitoe wito kwa wavuvi kutoa taarifa Serikalini ili kuepisha utokea kwa madhara yasiyotarajiwa , baada ya kuhifadhi majumbani mwenu ” alisisitiza Mkuu wa Wilaya.
Mmoja wa mashuhuda waliookota bawa hilo Chungua Hamad Chungua aliishauri mamlaka ya Usafiri wa Anga kuwaandalia mazingira mazuri ya kuwapatia mashine ya uvuvi ambayo itawasaidia katika kazi zao za uvuvi .
Alisema , ni vyema Mamlaka hiyo kuwazawadia mashine ya supa kumi au kumi na tano kutokana na usumbufu walioupata wakati wa kulikokota kwani ni zito na bahari ilikuw aimechafuka .
Hata hivyo Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga iimekabidhi shilingi milioni mbili wavuvi waliofanikisha kuliokota na kulihifadhi kama ni zawadi .
Kwa mujibu wa taratibu na sheria , Mamlaka ya Usafiri wa Anga haina ulazima wa kuwalipa wananchi wanaokota vitu aidha baharini au nchi kavu , isipokuwa hulazimika kutoka zawadi ili kuwajenga imani wananchi ya kuvihifadhi vitu wanavyo viokota
No comments:
Post a Comment