Saturday 2 July 2016

RAIS WA RWANDA, PAUL KAGAME AKABIDHI TUZO KWA WASHINDI SABASABA

HERM7530
Rais wa Rwanda, Paul Kagame (wa pili kulia) akimkabidhi tuzo ya Mshindi wa Tatu Sekta ya Mawasiliano na Tehama (ICT) Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Prof. Tolly Mbwette (kushoto) kwenye maonesho ya 40 ya Kimataifa ya Biashara viwanja vya Mwalimu Nyerere sabasaba jijini Dar es Salaam.

Kulia ni Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli na Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage (wa pili kushoto)

Na. Immaculate Makilika, MAELEZO
RAIS wa Serikali ya Rwanda Mheshimiwa Paul Kagame amewakabidhi tuzo  kwa Wizara, taasisi za Serikali, kampuni, nchi washiriki pamoja na mashirika yaliyoshinda katika maonesho ya 40 ya biashara ya kimataifa.
Rais Paul Kagame alikabidhi tuzo  hizo jana, wakati alipokuwa akifungua maonesho ya 40 ya biashara ya kimataifa katika viwanja vya Mwl Nyerere maarufu kama Sabasaba, vilivyopo katika barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam.
Wizara na taasisi za Serikali, kampuni pamoja na mashirika mbalimbali yalishiriki maonesho hayo kwa kushindana katika kuonesha bidhaa bora  na kueleza huduma nzuri  wanazotoa, ambapo baadae Rais Paul Kagame aliwakabidhi washindi hao tuzo mbalimbali.
Baadhi ya  washindi hao walioganywa katika makundi mbalimbali ni pamoja na,  kundi la bidhaa za kilimo nafasi ya mshindi wa tatu ilishikwa na  kampuni ya farm equip Tanzania limited, nafasi ya mshindi wa pili ilishikwa  na  kampuni Asas dairies na nafasi ya  mshindi wa kwanza ilishikwa na  Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT).
Katika kundi la usindikaji wa vyakula na huduma za vinywaji, nafasi ya mshindi wa tatu ilishikwa na kampuni ya  Bakhresa Group, ikifuatiwa na kampuni ya P&P, na nafasi ya  mshindi wa kwanza ilishikwa na  kampuni ya Afri tea and coffe blenders limited.
Kwa upande wa taasisi za kifedha, nafasi ya mshindi wa tatu ilishikwa na  benki ya TIB, ikifuatiwa na Benki ya CRDB huku Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ikishika nafasi ya  kuwa  mshindi wa kwanza. Vilevile katika kundi la Mifuko ya hifadhi ya jamii nafasi ya mshindi wa tatu ilishikwa na mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF, nafasi ya mshindi wa  pili ilishikwa na Mfuko wa Pensheni wa  LAPF na nafasi ya mshindi wa kwanza ikiwa ni Mfuko wa  Pensheni wa  PPF.
Kwa upande wa nchi za kigeni zilizoshiriki maonesho hayo ya 40 tuzo zilienda kwa nchi za Rwanda iliyoshika nafasi ya  mshindi wa tatu, Ujerumani ikishika nafasi ya mshindi wa pili huku  nafasi ya mshindi  wa kwanza ikiwa  ni nchi ya  Afrika Kusini. Aidha, washindi wa jumla walioshiriki katika  maonesho ya 40 ya biashara ya kimataifa ya Sabasaba ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kilichoshika nafasi ya mshindi wa tatu , ikifuatia  Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja Chuo cha Cha Ufundi  Stadi (VETA) kilichoshika nafasi ya mshindi wa kwanza.
Baada ya kuwakabidhi tuzo hizo na kufungua rasmi maonesho hayo ya 40 ya biashara ya kimataifa Rais Kagame alitoa wito kwa washiriki wa maonesho hayo ya 40, kushirikiana ili kubuni mawazo mapya ya biashara ikiwa ni pamoja na  kutambua fursa zilizopo katika soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, katika kukuza biashara zao na kusaidia ukuzaji wa uchumi wa pamoja katika nchi wanachama wa  Jumuiya hiyo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!