MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu watu watatu akiwamo raia wa Saudi Arabia, Alhamaidah Momouda, kulipa faini ya Sh. milioni 10 ama kwenda jela miaka mitano, baada ya kukutwa na hatia ya kosa la kusafirisha binadamu.





Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi, baada ya washtakiwa hao kukiri mashtaka dhidi yao.
Washitakiwa hao walishindwa kulipa faini na kupelekwa gerezani kutumikia kifungo.
Mbali na Momouda, washtakiwa wengine ni Raia wa Kenya, Ali Muhammed na raia wa Morocco, Dounia Benneni.
Hakimu alisema baada ya washtakiwa kukiri makosa yao, mahakama imewatia hatiani kwa kosa la kusafirisha binadamu kwani kosa hilo linatakiwa kupigwa vita na ili iwe fundisho kwa wengine.
“Mahakama hii inawatia hatiani kwa kosa hilo, kwa mujibu wa sheria kosa hili washtakiwa mtalipa faini ya Sh. milioni 10 kila mmoja ama mkishindwa mtakwenda jela kutumikia kifungo cha miaka mitano” alisema Hakimu Shahidi.
Hata hivyo, washtakiwa hao walishindwa kutimiza masharti hayo na walipelekwa gerezani kutumikia kifungo chao.
Mapema mahakamani hapo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Idara ya Uhamiaji, Method Kagoma, ulidai kuwa siku isiyofahamika kati ya Aprili 29 na Juni 6, mwaka huu, jijini Dar es Salaam,washtakiwa walikula njama ya kusafirisha binadamu.
Alidai tarehe ya tukio la kwanza, eneo la Kariakoo, wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, washtakiwa kwa pamoja waliwakusanya, kuwapokea na kuwasafirisha Irakoze Singorine, Rahma Girukishaka na Shimilimana Hassan, Nduimana Riziki, Rehema Cancana, Shimilimana Selemeni, Dunishe Bella, Irakoze Amana, Nizingimana Aisha, Inasuku Endru, Zawadi Niyonzima na Nzeyimana Amina, kutoka Dar es Salaam kwenda Saudi Arabia baada ya kuwadanganya kwamba wangewatafutia ajira huku wakijua wanawapeleka kuwatumikisha kazi za kitumwa.