Tuesday 5 July 2016

POLISI WASAKA ABIRIA TISA WALIOZAMA ZIWANI

VIKOSI vya uokoaji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma, vinaendelea na kazi ya kuwasaka abiria tisa, kati ya 45, waliozama maji baada ya kutokea kwa ajali ya boti katika Ziwa Nyasa juzi.


Hadi sasa watu 36 wameripotiwa kuokolewa kutokana na kazi kubwa, iliyofanywa na vikosi vya uokoaji vya Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi wanaoishi katika vijiji vya pembezoni mwa Ziwa Nyasa.
Chanzo cha habari kutoka eneo la tukio, kililiambia gazeti hili jana kuwa boti hiyo ilizama baada ya kugonga mwamba ndani ya ziwa hilo saa tisa alasiri jirani na kilipo kijiji cha Mkenda wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.
“Ni kwamba boti ilikuwa na jumla ya abiria 45, lakini hadi sasa ni abiria 36 ndio waliookolewa wakiwa hai na wengine tisa bado hawajajulikana mahala walipo.
Ilikuwa ikitokea katika kijiji cha Nakawale kuelekea kijiji cha Mitomoni.
“Ni vigumu sana kwa sasa kusema kama hao ambao hawajapatikana wamekufa maji au la, maana inawezekana wakawepo ambao baada ya kujiokoa walikimbia na kutokomea kusikojulikana kutokana na kiwewe,” kilisema chanzo hicho.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, abiria waliookolewa katika ajali hiyo walifikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma na kupatiwa matibabu na baadaye kuruhusiwa kwenda makwao kutokana na afya zao kutengamaa.
Habari zaidi kutoka eneo hilo la tukio, zilisema kuwa nahodha wa boti hiyo, Said Auyu alitokomea mahali kusikojulikana baada ya kujiokoa katika ajali hiyo.
Juhudi za gazeti hili kumpata Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji ili kuzungumzia tukio hilo kwa kina hazikuweza kupatikana kutokana na kile kilichooelezwa na wasaidizi wake kuwa alikuwa katika eneo la tukio, kufuatilia kazi ya kuwaokoa abiria ambao bado hawajapatikana.
“Hivi unavyozungumza na mimi, RPC (Mwombeji) amerudi tena katika eneo la tukio ili kuongeza nguvu ya kuwatafuta abiria tisa waliosalia na baada ya kukamilisha kazi hiyo atakuwa katika nafasi nzuri ya kuwapa taarifa za kina za ajali hiyo,” alisema mmoja wa wasaidizi wa RPC, ambaye hata hivyo hakuwa tayari kutaja jina lake.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!