Tuesday, 12 July 2016

Mgonjwa ICU amgundua daktari feki




JESHI la Polisi mkoani hapa linamshikilia Zacharia Benjamin (35) kwa tuhuma za kuingia katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro na kujifanya daktari.



Mtuhuhumiwa huyo ambaye aligunduliwa na mmoja wa wagonjwa waliolazwa katika wodi ya wagonjwa mahututi hospitalini hapo, baada ya kukamatwa alidai yeye ni mwanajeshi, askari mstaafu, polisi na pia aliwahi kuwa mganga wa hospitali, hivyo hazuiliwi kuingia popote anapotaka.
Akielezea tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Jumapili iliyopita saa 11 jioni katika Wodi ya Wagonjwa Mahututi (ICU) kwenye hospitali hiyo.
Alisema mtuhumiwa huyo huku akijua kufanya hivyo ni kosa, aliingia katika hospitali hiyo na kutembelea wodi zote tisa na baadae kuingia wodi ya wagonjwa mahututi.
Alisema, awali mtuhumiwa huyo alipofika wodi namba saba aliingia chumba cha manesi na kuchukua koti la mganga, kulivaa na kutembelea kuingia katika wodi hizo.
Akiwa katika wodi hizo, alisema Matei, mtuhumiwa alijitambulisha kuwa ni daktari mgeni anayekagua wagonjwa kama wanapata huduma ipasavyo.
Kamanda Matei alisema daktari huyo feki alipoingia ICU alianza kuwahoji wagonjwa, na ndipo mmoja aliyekuwa na nafuu kidogo alipopiga simu polisi na kutoa taarifa juu ya mtu huyo ambaye alikuwa akimshuku kuwa sio daktari.
Alisema polisi walipofika walimkamata na anatarajiwa kufikisha mahakamani mara upelelezi utakapokalimika.

Akizungumzia tukio hilo, Benjamin alidai alifika hospitalini hapo Jumapili iliyopita akiwa na mgonjwa wake ambaye amelazwa kwenye wodi namba nane na kisha kuondoka kuendelea na shughuli zake, na kwamba siku hiyo alipigiwa simu na mgonjwa wake kuwa hajapata huduma yoyote tangu afike hapo.
Taarifa hiyo, alisema, ndiyo iliyomafnya aamue kuingia hospitalini hapo kukagua hali ilivyo.
Mtuhumiwa huyo, pia alisema yeye ni mwanajeshi na askari wa zamani ambaye pia aliwahi kuwa mganga na daktari, mwenye ruhusa ya kuingia popote pale bila kuzuiliwa na mtu yeyote.
Akizungumzia tukio hilo, muuguzi wa zamu, Ester Uwiza, alisema mtu huyo aliingia wodi namba moja akiwa hana koti la udaktari na baadaye akaenda wodi namba saba na kuingia chumba cha kubadilishia nguo ambako alichukua koti la daktari na kulivaa na kwenda chumba namba tisa kabla ya kukamatwa.
Maganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Frank Jacob, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataka wananchi kuwa makini na watu wanaojitambulisha kuwa ni madaktari na kwamba wameweka mikakati ya kuhakikisha wanawabaini wanaojifanya madaktari katika hospitali na vituo vya afya mkoani humo.
Hii ni mara ya pili Hospitali ya Rufaa Mko wa Morogoro kukamata watu wanaojifanya kuwa ni madaktari wakati hawana ujuzi wala uelewa wa taaluma hiyo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!