MENEJA wa kiwanda cha biskuti cha Simba, kilichoko jijini hapa, Suresh Naranjian Somaiya (72), amekutwa amekufa akiwa na kamba ya kiatu shingoni.
Somaiya mwenye asili ya Asia na mkazi wa Mtaa wa Barabara ya Nyerere, mwili wake ulikutwa ukiwa na jeraha dogo upande wa bega la kushoto, jambo lililosababisha kifo chake kielezwe kuwa ni cha kutatanisha.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Julai 9, mwaka huu, saa 10:00 alfajiri katika Mtaa wa Barabara ya Nyerere.
Alisema alikutwa amekufa kwenye nyumba yake aliyokuwa akiishi na mdogo wake wa kiume, shemeji yake na msichana wa kazi za ndani (majina yamehifadhiwa).
“Ilipofika majira ya usiku, mdogo wake huyo wa kiume aliyekuwa anaishi naye, alipokwenda chooni alimkuta kaka yake akiwa ameanguka na amekufa ndipo alipotoa taarifa Polisi”, alisema.
Alisema Polisi walifika katika eneo la tukio na kukuta mwili wa marehemu ukiwa na jeraha dogo begani ukiwa umefungwa kamba ya kiatu shingoni.
"Tunafanya uchunguzi wa chanzo cha kifo hicho. Aliongeza kuwa Polisi inawahoji ndugu na jamaa wa marehemu waliokuwa wanaishi naye. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Bugando kwa ajili ya uchunguzi ”, aliongeza.
Kamanda Msangi aliwataka ndugu na jamaa wa marehemu kuwa watulivu ili Polisi ifanye uchunguzi wake kuhusu chanzo cha kifo hicho.
“ Ikithibitika kuna mtu au watu wamehusika kwenye tukio hili hatua zinazostahili za kisheria zitachukuliwa dhidi yao”, alisema.
No comments:
Post a Comment