Tuesday 19 July 2016

Makonda: Sijasema wasio na kazi wakamatwe



Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
 Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa ufafanuzi wa shughuli ya sensa ili kubaini watu wasiokuwa na kazi, akisema hajatamka wasio na kazi wakamatwe.



Akihojiwa jana katika kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na Redio Clouds, Makonda alisema watu hawakuelewa lengo la sensa hiyo.

Makonda alisema lengo la kuwatambua watu wasiokuwa na kazi ni kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema anacholenga katika sensa hiyo, ni kwa ajili ya usalama wa mkoa ili kila mtu ajulikane shughuli anayoifanya. Aliongeza kuwa ameshangaa kusoma kwenye mitandao ya jamii, watu wakijadili mambo ambayo hajawahi kuyatamka.
Makonda alisema alipoteuliwa na Rais John Magufuli kuwa mkuu wa mkoa na mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama, alifanya mkutano na wenyeviti wa mitaa.
Alisema katika mkutano huo, aliwaeleza wenyeviti hao kuwafahamu vizuri watu kwenye mitaa wanayoiongoza, akiwataka wajue kazi wanazozifanya wananchi wao kwa ajili ya usalama.
Tangu kuibuka kwa sakata hilo, kumekuwa na majadiliano yanayoendelea katika mitandao ya jamii kuhusu kauli ya Makonda ya msako wa nyumba kwa nyumba kuwabaini vijana wasiokuwa na kazi, huku wengi wao wakilalamikia tamko hilo.
Kuhusu kuondoa ombaomba, Makonda alisema ataendelea na kazi hiyo ili watoto wanaoomba wajiunge na shule za msingi.
“Rais John Magufuli ametoa nafasi kwa watoto hawa kusoma bure, lakini wao wapo barabarani wanaomba, hivi kuwapa fedha ni kuwasaidia?” alihoji.
Makonda alisema watoto wengi wanatumikishwa katika kazi ya kuomba na watu ambao siyo ndugu zao.
“Yaani wao wanaomba lakini mtu mwingine ndiye anachukua fedha hizo, natoa wito jamii inisaidia kwa kutowapa fedha ombaomba hawa,” alisema Makonda. Alisema shughuli ya kuwaondoa ilianza Juni na kwamba mwezi ujao atatoa tathmini ili kuona kama imefanikiwa au la.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!