Tuesday, 26 July 2016

MAALIM SEIF KUNGURUMA TENA MAREKANI

Na Mwandishi wetu,  Philladelphia
Makamo wa Kwanza Mstaafu wa Rais wa Zanzibar na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, anatazamiwa kunguruma tena chini Marekani wiki hii.
Maalim Seif Sharif Hamad  akiwasili katika uwanja wa ndege Philladelphia
Gwiji huyo wa siasa ambaye aliwasili jijini Philladelphia hapo jana, anatarajiwa kuwakhutubia Watanzania katika Mkutano wa hadhara utakaofanyika Jumamosi hii katika jiji la Boston.


Katibu huyo Mkuu wa CUF pamoja na ujumbe anaofuatana nao aliwasili nchini humu akitokea Uingereza baada ya kukamilisha ziara yake ya Ulaya iliyochukua muda wa zaidi ya wiki moja. 
Akiwa Ulaya Maalim Seif alitembelea Uiengerza na kufanya mikutano na Maofisa wa ngazi za juu wa Serikali ya Uingereza, Vyama vya kisisasa na Taasisi mbalimbali. Baadaye alielekea nchini Ubelgiji ambako alifanya ziara kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Ulaya na kufikisha madai ya Wazanzibari ya kurejeshewa haki yao ya Kidemokrasia.
Aidha alitembelea nchini Uholanzi ambako pamoja na mambo mengine, alikutana na maofisa wa Mahakama ya Ukhalifu ya Kimataifa na kufikisha kilio cha Wazanzibari dhidi ya Uvunjaji wa Haki za Binadamu unaendelea Visiwani Zanzibar.
Ziara hiyo ya Ulaya ilikuja katika kile maofisa wa CUF walichokielezea kuwa ni awamu ya pili ya ziara za nje za mwanasiasa huyo mkongwe katika juhudi za kutafuta uungwaji mkono wa Kimataifa kwa mgogoro wa Kisiasa Zanzibar.
Maalim Seif ambaye anafuatana na Mkuuwa Watumishi katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa CUF Bwana Issa Kheir Hussein, yupo nchini Marekani kuitikia mwaliko wa kuhudhuria kwenye Mkutano Mkuu wa Chama Cha Democratic ulioanza jana jijini Philladelphia, mkutano ambao unatazamiwa kumpitisha Bi Hillary Clinton kuwa mgombea wa Urais wa Marekani kwa kuoitia tiketi ya Chama hicho.
Katika mkutano wake wa hadhara na Watanzania, Maalim Seif, aliyekuwa mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha CUF katika uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba mwaka jana, anatazamiwa kuzungumzia zoezi zima la uchaguzi huo uliofutwa, na kusisitza madai ya Chama chake ya kurejeshewa haki yao waliyoporwa katika uchaguzi huo, na mwenendo mzima wa Demokrasia nchini Tanzania.
Itafaa kukumbusha kuwa hii ni mara ya pili kwa Maalim Seif kuzuru Marekani katika kipindi cha chini ya miezi miwili. Mwezi uliopita, Maalim Seif alikuwepo nchini humu na kufanya mazungumzo na viongozi wa Kisiasa na mashirika binafsi, na kutembelea Umoja wa Mataifa ambako alifikisha madai ya Chama chake ya ukandamizaji wa demokrasia nchini Tanzania. Aidha alizungumza na Watanzania waishio nchini Marekani katika jiji la Washington.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!