Wafanyabiashara Mohamed Mustafa Yusufali (kulia), na Samuel Lema (kushoto).
MFANYABIASHARA Mohamed Mustafa Yusufali maarufu kama Mohamedali ama Choma au Jamalii, ambaye ni mshitakiwa namba moja na mbuili katika kesi mbili tofauti.
Jana amesomewa mashtaka 186 na kufanya idadi ya mashtaka yanayomkabili katika kesi hizo za kuhujumu uchumi kufikia 383, yakikiwamo ya kughushi, kuisababishia hasara Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kukwepa kodi na kutakatisha fedha.
Jana Yusufali alipandishwa kizimbani kwa pamoja na mfanyabiashara maarufu wa jijini Arusha, Samwel Lema wakikabiliwa na mashtaka 222, ikiwamo moja la kula njama, 218 ya kughushi, kukwepa kodi, kutakatisha fedha na kuisababishia TRA hasara ya zaidi ya Sh. bilioni 14.
Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Wilbard Mashauri.
Mapema mwezi huu, Yusufali na wenzake walifikishwa katika mahakama hiyo wakikabiliwa na mashtaka 199 ikiwemo 181 ya kughushi, 15 kuwasilisha nyaraka za uongo, kukwepa kodi, kutakatisha fedha na kuisababishia hasara Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), hasara ya Sh. bilioni 15.6.
Kati ya mashitaka hayo 199, Yusufali alikabiliwa na 197 na mengine yakiwahusu Alloyscious Mandago, Isaack Kasanga, Taherali Taherali na Mohamed Kabula, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi.
Katika kesi ya jana, upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi, Mawakili wa Serikali Jackline Nyantori, Diana Lukondo na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Leonard Swai.
Upande wa Utetezi uliongozwa na Mawakili Alex Mgongolwa, Omary Omary, Hudson Ndusyepo na Nehemia Nkoko.
Kishenyi alidai katika shtaka la kwanza, kati ya Januari Mosi mwaka 2012 na Desemba 31, mwaka 2014 katika jiji la Arusha na Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja walikula njama ya kuidanganya TRA kwa lengo la kujipatia Sh. bilioni 14.
Upande huo wa Jamhuri, ulidai katika shtaka la pili hadi la 103, katika tarehe tofauti wakiwa na nia ovu watuhumiwa walitengeza hati za malipo ya kodi za uongo zenye thamani tofauti ya fedha, kwamba Kampuni ya Northern Engineering imenunua kutoka kwa Festive General Business Limited huku wakijua siyo kweli.
Nyantori alidai shtaka la 104 hadi la 141 na shtaka la 220, yanamkabili Lema peke yake, na kwamba katika tarehe tofauti jijini Dar es Salaam, mshtakiwa huyo alitengeneza hati za malipo ya kodi za uongo akionyesha kwamba Kampuni Northern Engineering Works Ltd, imenunua bidhaa huku wakijua siyo kweli.
Kampuni nyingine zinazodaiwa kutengenezewa hati za uongo ni Elerai Constructions Co Limited, kwamba imenunua kutoka kwa Blue Arrow Tanzania Limited, Northern Engineering imenunua kutoka Ever Global General Trading Limited, Elective General Co. Limited, Great Lake Supplies Limited, Akberali General Supply Ltd, Cebers General Company, Adam Geral Trading Limited na Farm Plant Procurement Logistics Limited.
Kampuni nyingine zilizotengezewa hati za malipo ya kodi za uongo ni Northern Engineering imenunua kutoka kwa Royal International Limited, Elerai Construction Co. Limited, imenunua kutoka kwa Blue Arrow Tanzania Limited, Kitonga General Hardware, Jupitar General Supplies, Raneys General Enterprises Limited, Coatblue General Co. Limited.
Nyingine ni, Northern Engineering Works Ltd imenunua kutoka kwa Profen International, Farmplant Dsm Limited, Phase Enterprises Limited, Profen International, Kampuni ya Elerai Comstruction Co. Ltd imenunua kutoka kwa Auct Ltd, Jamco
Agencies, Tulime General. Mandela Equipment & Logistics Co. Ltd, Rafiki Commidities (T) Ltd na Almis Trading Company Limited.
Swai alidai katika shtaka la 220, kati ya Januari Mosi mwaka 2012 na Desemba 31, mwaka 2015 jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Lema akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Northern Engineering Works Limited na Elerai Construction Ltd aliwasilisha kwa Kamishna wa Kodi nyaraka za uongo akionyesha kwamba kampuni hizo zimesajiliwa kihalali na zimelipia kodi ya Sh. 14,052,011,435.69.
Katika shtaka la 221, ilidaiwa kuwa kati ya Februari Mosi mwaka 2012 na Februari 25, mwaka 2013, jijini Arusha na Dar es Salaam, watuhumiwa walifanya utakatishaji Sh. milioni 420 zilizoingizwa kwenye akaunti ya Iqbal Jaferali Jafferjee iliyopo benki ya I&M (T) Ltd tawi la Kariakoo.
Katika shtaka la 222, ilidaiwa kuwa Januari Mosi, mwaka 2012 na Desemba 31, mwaka 2015 jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja waliisababishia hasara TRA ya Sh. bilioni 14 mali ya mamlaka hiyo.
Hakimu Mashauri alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi mpaka upelelezi utakapokamilika itahamishiwa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Wakili Mgongolwa alidai kuwa shtaka la kutakatisha fedha lina mapungufu ya kisheria na kwamba utetezi unaomba mahakama hiyo kuliondoa.
Upande wa Jamhuri uliomba siku moja kwa ajili ya kupitia vifungu vya sheria kujibu pingamizi la utetezi.
Hakimu alisema mahakama yake itasikiliza hoja za Jamhuri kesho.
NIPASHE.
No comments:
Post a Comment