Wednesday, 20 July 2016

HAYAKUHUSU! BARUA YA WAZI KWA DIAMOND!

diamond

KWAKO King wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’. Habari za siku ndugu yangu. Vipi familia yako yote haijambo?


Ukitaka kunijulia hali, mimi sijambo. Ni mzima wa afya. Naendelea kupambana ndani ya mjengo huu mkubwa wa magazeti Pendwa, Global Publishers. Hapa sisi ni kazi tu. Kuhabarisha, kuburudisha na kuelimisha jamii yetu.
Madhumuni ya kukuandikia barua hii kwanza kabisa ni kukupongeza. Kwa kila mwenye akili timamu yenye kuwaza kwa mlengo chanya wa Muziki wa Bongo Fleva, kamwe hawezi kuacha kupongeza kazi nzuri uliyoifanya na wale mapacha kutoka Nigeria, P-Square.
Umewakimbiza. Umeonesha unajua kuimba na kucheza zaidi yao. Harakati zako unazozifanya kila siku katika kuhakisha unapiga hatua wewe binafsi na Bongo Fleva kwa ujumla ni mpuuzi pekee anayeweza kukupinga na kusema labda hufai.
Unajua kuandaa muziki na kuuachia kwa wakati. Una timu nzuri ambayo inakujenga kistaa kwa kufuata au kujifunza kutoka kwa watu mbalimbali waliofanikiwa kimuziki. Ninapokupongeza kuhusu suala la kujifunza kutoka kwa waliokutangulia, hapo pia kuna msingi wa barua yangu.
Niwe mkweli ndugu yangu, sijafurahishwa na namna ambavyo ulijirekodi video zenye mlengo wa kujidhalilisha ili tu kutengeneza ‘awareness’ ya wimbo wako. Ukaamua kuingia bafuni, wewe na mpenzi wako mkayafanya yale mliyoyafanya.
Binafsi najua hata yale uliyoyafanya, umeiga. Yawezekana ni wewe au uongozi wako ulikupanga wewe kufanya vile ili kutengeneza ile kiki lakini kitu cha msingi ninachotaka kukuambia, lazima utambue utamaduni wetu pia.
Kuna kiki nyingine haziendani na utamaduni wetu. Masuala ya kuonesha mambo mliyoyafanya faragha, kwa mila na destuli zetu za Kitanzania, haipendezi. Watanzania wanajua kuiheshimu faragha. Mbona kuna vitu vingi unaweza kufanya na vikatengeneza kiki?
Bahati nzuri wewe watu wanakuelewa. Hauhitaji kufanya vitu vya kujidhalilisha saana ili waweze kukuzungumza. Yale mambo ya wewe kumlamba mpenzi wako kwapani huku unakula, siyo ishu. Watu wengi wanayafanya tena pengine zaidi ya yale lakini kamwe hawawezi kuyaweka kwenye mitandao.
Kwanza ni kujidhalilisha, pili ni kujishushia heshima wewe na huyo mpenzi wako. Watu wanaojua zaidi ya ulivyofanya pia wanaweza kukucheka na kukuona pengine hujui. Au wanaweza kusema wewe mshamba wakati wewe si mshamba. Una maana yako.
Maana yako ifanye katika njia ambazo haziwezi kuharibu Utanzania wako. Wewe una watu wanakuheshimu. Una wazazi, una jamii kubwa tu inayokuheshimu wakiwemo hata viongozi wa kiserikali, unapofanya mambo ya aina hiyo yanaweza kukukosesha hata baadhi ya michongo ya kazi.
Ni matumaini yangu utakuwa umenielewa na utaufanyia kazi ushauri wangu. Nakupongeza na pia nakuomba ubadilike.
Mimi ni ndugu yako;

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!