Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa, ambayo Mwenyekiti wake ni Mkaguzi na Mdhibiti n Mkuu wa Hesabu za Serikali, ( CAG) Profesa Mussa J. Assad jana ( Jumanne) imerejea na kuidhinisha ripoti kumi na moja za Mashirika, Mifuko na shughuli mbalimbali za Umoja wa Mataifa.
Katika kikao hicho cha 70 kilichofanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, pamoja na kuidhinisha ripoti za Mashirika na Mifuko iliyochini chini ya Umoja wa Mataifa, pia Bodi ilipokea taarifa mbalimbali za kiutendaji zinazohusiana na majukumu ya Bodi hiyo.
Wajumbe wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa, ni Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu wa Serikali ya India, Bw. Shashi Kant Sharma, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Uingereza, Sir Amyas Morse, na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Prof. Mussa J. Assad.
Pamoja na kupitia na kuridhia ripoti hizo kumi na Moja, na kupokea taarifa za kiutendaji, shughuli nyingine iliyofanywa na Bodi ya Ukaguzi ilikuwa ni pamoja na kuiaga Ofisi ya Ukaguzi ya Uingereza baada ya kumaliza kipindi chake cha miaka sita ya uhudumu katika Bodi hiyo.
Hafla ya kuagwa kwa Ofisi ya Ukaguzi ya Uingereza ilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Ban Ki Moon pamoja na wadau mbalimbali ambao ni wateja wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa.
Nafasi ya Ofisi ya Ukaguzi ya Uingereza imechukuliwa na Ofisi ya Ukaguzi ya Ujerumani ambayo imekaribishwa rasmi kuwa mjumbe wa Bodi hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo ya kuiaga ofisi ya Ukaguzi ya Uingereza na kuikaribisha Ofisi ya Ukaguzi ya Ujerumani, Mwenyekiti wa Bodi, Prof. Mussa Assad amemshukuru Sir. Amyas Morse kwa mchango wake yeye binafsi na Ofisi yake kwa uwajibikaji mkubwa na weledi wa hali ya juu ambao umefanikisha utekelezaji wa mamlaka na majukumu ambayo Bodi hiyo imekabidhiwa na Umoja wa Mataifa.
Akiikaribisha Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Ujerumani, Prof. Assad ameelezea matumaini yake ya kufanya kazi kwa karibu na ushirikiano wa hali ya juu na mjumbe huyo ili kwa pamoja waweze kutekeleza majukumu na mamlaka waliyokabidhiwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa, ilianzishwa mwaka 1946 na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa lengo la kukagua hesabu za Mashirika, Mifuko na Taasisi nyingine zilizo chini ya Umoja wa Mataifa, ili pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba Taasisi hizo zinatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa kanuni na taratibu za Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na matumizi yenye tija na adilifu ya bajeti kulingana na mamlaka ya Mashirika na Taasisi hizo.
Bodi ya Ukaguzi inatekeleza majukumu yake kama chombo huru na taarifa zote za ukaguzi huwasilishwa kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pamoja na wateja ambao wanakaguliwa na Bodi hiyo.
No comments:
Post a Comment