mama akimnyonyesha mtoto wake.


CHANGAMOTO ya kuboresha hali ya lishe kimsingi ni moja ya mambo yanayoihusu dunia nzima, katika karne hii ya 21.

Karibu kila nchi duniani kwa njia moja ama nyingine, ina kiwango cha utapiamlo kinachotishia afya ya wananchi wake
.


Kwa mujibu wa takwimu za hali ya lishe duniani, kwenye Ripoti ya Lishe ya Dunia iliyotolewa mwaka 2014 (Global Nutrition Report), kati ya watu bilioni mbili hadi tatu duniani wana utapiamlo.

Ripoti hiyo ilitolewa na Kundi la Wataalamu Huru (IEG), lililokasimiwa mamlaka na wadau wa lishe.
Dunia hivi sasa ina watu takriban bilioni 7.4 kwa mujibu wa takwimu za asasi ya Worldometers.

Kwa maana hiyo, wanapozungumziwa kati ya watu bilioni mbili na tatu wenye utapiamlo kwa kuitafasiri ripoti ya hali ya lishe ya dunia ya mwaka 2014, ina maana kwa kila watu saba, wawili au watatu kati yao wana utapiamlo.
Ni ugonjwa unaoonekana katika mifumo mbalimbali kama vile; lishe duni, unene uliopitiliza au uzito mkubwa na upungufu wa madini mwilini mwa watu.
Inaelezwa kuwa, kati ya kila watu saba, wawili hadi watatu kati yao ana utapiamlo. Ni suala linaloonyesha ukubwa wa tatizo linaloikabili dunia kwa sasa.
Hiyo maana yake ni kwamba, kila walipo Watanzania saba, kati yao wawili na watatu wana utapiamlo.
Hiyo ni moja ya jitihada za pamoja za dunia, ikiwamo Tanzania kuchukua hatua ya kukabiliana na janga hilo.
MKURUGENZI WA PANITA
Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Lishe Tanzania (PANITA), Tumaini Mikindo, anasema kwa kutambua uzito wa tatizo hilo, mwaka 2012, Baraza la Afya Duniani (WHA), lilipitisha Malengo ya Lishe kufikia mwaka 2025.

Aidha, ilipitisha malengo hayo kupitia azimio namba 65.6, na Tanzania ilikuwa kati ya nchi zilizounga mkono.
“Malengo hayo ni pamoja na kupunguza idadi ya watoto waliodumaa wenye umri chini ya miaka mitano kwa asilimia 40; kupunguza kiwango cha upungufu wa damu kwa wanawake walio katika umri wa uzazi kwa asilimia 50,” anasema na kuongeza:
“Aidha, kupunguza kiwango cha watoto kuzaliwa wakiwa na uzito pungufu kwa asilimia 30, na kuzuia kuongezeka kwa tatizo la uzito uliozidi miongoni mwa watoto.”
Malengo mengine anayoyataja Mikindo, ni kuongeza kiwango cha unyonyeshaji watoto maziwa ya mama tu kwa miezi sita ya mwanzo kwa walau asilimia 50 na kupunguza tatizo la ukosefu wa lishe kwa watoto.
Aidha, anasema Tanzania ilitia saini kwenye Malengo ya Kikao cha Umoja wa Afrika cha Malabo, Guinea Ikweta mwaka 2013, ikilenga kupunguza udumavu kufikia chini ya asilimia 10 ifikapo 2025, yaani miaka tisa kuanzia sasa.
Mbali na hayo, Mikindo anasema mwaka 2013, viongozi wa nchi zote duniani walikutana jijini London, Uingereza, kwenye Mkutano wa Kwanza wa Lishe kwa Maendeleo (Nutrition For Growth Summit-N4GI), ambako Rais mstafau Jakaya Kikwete, alihudhuria, akiwa na ujumbe wake wakiwamo viongozi na maofisa waandamizi wa serikali.
Anasema wawakilishi hao waliweka dhamira kwa nchi husika, kutenga rasilimali na kuhakikisha malengo ya kuboresha hali ya lishe ifikapo mwaka huo wa 2015 yanafanikiwa.
“Baada ya tathmini, mkutano huo uliona kwamba ili malengo hayo yaweze kutimia, kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano, anahitaji kutengewa bajeti ya Dola za Marekani 8.5 kwa mwaka, ambayo ni watani wa Sh. 19,000 za Kitanzania katika bajeti ya taifa,” anasema.
TATHMINI YA BAJETI YA LISHE
Mtazamo uliopo ni kutathmini hali ya lishe nchini, ikioanishwa na malengo yaliyowekwa, ambayo yako makuu matatu yanayozaa maswali;

Kwanza, ni athari zake kwa binadamu kiafya na kiuchumi.
Pili, namna serikali ya inavyojidhatiti kukabiliana na utapiamlo, kwa mujibu wa malengo yaliyowekwa na WHA mwaka 2012, yanayotakiwa kuwa yametekelezwa ifikapo mwaka 2025, ambayo ni aka tisa kuanzia sasa.
Tatu, ni kutathmini ya fedha zilizotengwa, Sh. 19,000 kwa mwaka kama inakidhi haja.
ATHARI KIUCHUMI
Asilimia 45 ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano, vinachangiwa na utapiamlo. Lakini pia upungufu wa lishe, unasababisha zaidi ya asilimia 50 ya ulemavu wa muda mrefu kwa watoto chini ya miaka minne.

Kiuchumi, zuio la utapiamlo kwa mtoto, unaongeza asilimia 20 ya pato lake la saa na ongezeko la kiwango cha mshahara cha asilimia 33 zaidi.
Pia kwa kila fedha inayowekezwa kwenye lishe, utafiti unabainisha hurejesha faida ya mara 13.
Takwimu zote hizo ni kama zilivyobainishwa kwenye Ripoti ya Lishe ya Mwaka 2014.

UTAPIAMLO TANZANIA
Kwa mujibu wa takwimu za utafiti uliofanyika mwaka 2014 na taasisi ya Smart, hali ya utapiamlo hivi inapungua kwa mujibu wa takwimu za kimkoa, ikilinganishwa na utafiti wa Demografia na Afya (TDHS), uliotolewa mwaka 2010.

Kwenye utafiti huo wa TDHS, mkoa wa Dodoma ulikuwa na kiwango cha juu kuliko mikoa yote kwa utapiamlo, ukiwa na asilimia 56; Dar es Salam inafuatia kwa asilimia 19.
Lakini Smartb kupitia utafiti wa wa mwaka 2014, mkoa wa Kagera ndio ulio na kiwango cha juu cha utapiamlo kwa kiwango cha asilimia 52, wakati Dar es Salaam ikiendelea kuwa na kiwango cha chini cha utapiamlo kwa asilimia 16.
Ni jambo linaloonyesha kuna jitihada zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, katika kukabiliana na tatizo hili.
Hata hivyo haina maana utapiamalo umekwisha, tawimu zinaonyesha bado kiwango cha utapiamlo uko uko juu.
Madhara ya utapiamlo nayo yanaendelea kuathiri jamii ya Watanzania na hasa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
WIZARA YA AFYA
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Vincent Assey, anasema kuwa utapiamlo unaathiri ukuaji wa mwili na akili ya mtoto na usiposhugulikiwa katika kipindi cha miaka miwili ya ukuaji wake, madhara yake huwa hayatibiki maishani.

Dk. Assey anasema, utapiamlo husababisha magonjwa mengi yakiwamo ya akili, upungufu wa damu, vichwa vikubwa na
tezi la shingo.

Aidha, kuharibika kwa mimba kwa kinamama, watoto kuzaliwa wakiwa vilema, kukosa tija kwenye shughuli za kiuchumi na kukosa ubunifu na anasema kuwa utapiamlo unadhoofisha uchumi na kuleta udumavu wa kiafya.
“Kutokana na utapiamlo, wakulima hushindwa kutumia nguvu, na hivyo kusababisha mavuno kidogo na kupungua kwa tija ya wafanyakazi,” anafafanua
Dk. Assey anasema utapiamlo unachangia katika upotevu wa fursa za kiuchumi, kwani watu wazima wenye ukuaji uliodumaa wa ubongo kutokana na kukosa virutubisho kipindi cha utoto wana uwezo mdogo wa kubuni na kuchangamkia fursa mpya za maendeleo.
BAJETI YA LISHE
Kwa mujibu wa Dk. Assey, serikali imeweza kugharimia kupata watalaam wa lishe na kwamba kwa hivi sasa kuna maofisa lishe katika wilaya na halmashauri zote, kwa kiwango kinachofikia asilimia 93.

“Lakini tunataka kuwafika kule waliko wananchi wenyewe, kwani ndiko lishe inakotakiwa na kwa hali hiyo, tayari serikali imekubali tuanzishe mchakato wa kuajiri wahudumu wa afya wa jamii, watakakuwa kwa wananchi moja kwa moja,” anasema.
Kuhusu bajeti ya serikali, Dk. Assey anasema wako nyuma, lakini kuna hatua zilizochukuliwa kwa kila halmashauri kutenga Sh. 500 katika bajeti ya mwaka uliopo wa fedha, kushughulikia lishe ya watoto.
“Kiasi hicho ni cha kuanzia katika kufikia lengo lilopitishwa na N4GI,” anasema Dk. Assey.
WADAU
Michael Kehongoh kutoka shirika linalotetea haki za watoto nchini la C-Sema anasema, pamoja na halmashauri nchini kutakiwa kutenga Sh. 500 kwa ajili ya lishe, kiasi hicho hakitioshi na ni muhimu kikaongezwa zaidi katika siku zijazo.

Milembe Bukwimba, ambaye ni mkazi wa kijiji cha Ilamata, Kata ya Kulimi wilayani Maswa, mkoa wa Simiyu, anahimiza umuhimu wa serikali kupeleka wataalam hadi ngazi ya vijijini, ili wakawaelimishe wananchi na hasa kinamama, juu ya namna ya kuwapa lishe bora watoto wao.