Dar er Salaam. Kijana Abdullatif Hamisi (23), amemwandikia barua Jaji Mkuu akilalamikia hatua ya Mahakama Kuu kutoa hukumu mbili tofauti na kumnyima haki ya kupata mgawo wa urithi wa mali ya baba yake.
Hamis amemweleza Jaji mkuu kuwa yupo hatarini kupoteza haki yake ya urithi aliyoipigania tangu 2006 baada ya baba yake, Mohamed Hamis kufariki dunia.
Alisema nyumba ya baba yake ya ghorofa mbili iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam kwenye kiwanja namba 9 kitalu ‘A’ Mtaa wa Aggrey ikiwa na hati ya umiliki namba 56967, imeuzwa kwa Sh400 milioni.
Hata hivyo, Hamisi alidai pamoja na kushinda kesi Mahakama Kuu iliyoamuru apewe mgawo wake katika mauzo hayo, Mahakama hiyo hiyo kitengo cha Ardhi imempoka tena haki hiyo.
Kwa mujibu wa hukumu ya kitengo hicho cha Ardhi iliyotolewa na Jaji Fredrica Mgaya, Desemba 23, 2015, nyumba hiyo ya urithi sasa ni mali ya mfanyabiashara, Mehboob Yusuf Osman.
Mkataba wa mauziano kati ya mmoja wa wasimamizi wa mirathi unaonyesha moja ya sharti la mauziano hayo ni kwa msimamizi huyo naye kupewa sehemu (apartment) katika nyumba hiyo. Hata hivyo, Sheria ya Mirathi inakataza msimamizi wa mirathi kuwa mnufaika wa mali za marehemu.
Nyaraka za kimahakama ambazo gazeti hili inazo zinaonyesha mkataba wa mauziano ulifanyika mwaka 2006, lakini haionyeshi kama kuna mahali ambako msimamizi alishatoa taarifa hizo wakati kesi ikiendelea kortini.
Kutokana na mgongano huo, Hamis amemwandikia barua Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande akimuomba afanye mapitio ya dharura kwenye jalada la kesi hiyo ili kuepusha haki yake kupotea.
No comments:
Post a Comment