Saturday, 11 June 2016

WAOMBAO KAZI BILA KUPATA NCHINI SASA WAFIKIA 700, 000




Waombao kazi bila kupata nchini sasa wafikia 700,000
WAKATI Serikali ikiendeleza juhudi za kupambana na tatizo la ajira, ongezeko la watu wanaotafuta ajira kila mwaka nchini sasa limefikia 800,000, imefahamika.



Na kati ya watu hao (800, 000), ni 100,000 tu ndiyo hupata nafasi za kuajiriwa huku wengine 700,000 wakikosa fursa hiyo.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Tafiti kutoka Taasisi ya Kupunguza Umaskini (Repoa), Dk. Abell Kinyondo, wakati akizungumza na Nipashe kuhusu ripoti ya mapitio ya sera ya ajira ya mwaka 2008, ambayo waliipitia kwa lengo la kuangalia upungufu na kuboresha mambo yanayotakiwa kutafutiwa ufumbuzi ili kumaliza tatizo la ajira.
Dk. Kinyondo alisema lengo ni kuboresha sera ya ajira ya mwaka 2012 kupitia kwa wadau mbalimbali ambao wamewafikia tangu kuanza kwa utafiti huo mwaka jana; ambao ni wafanyakazi, waajiri, waajiriwa na wajasiriamali ili kuangalia mambo ya kurekebishwa katika sera ijayo.
“Licha ya namba ya watu ambao hawajaajiriwa kupungua kutoka asilimia 11 hadi 10, bado kuna tatizo la ongezeko la watu 800,000 kila mwaka ambao hawana ajira hali ambayo inasababisha tatizo hili kuzidi kukua,” alisema na kuongeza kuwa;
“Hii inatokana na watu wengi wanaozaliwa kila mwaka na ndio sababu kila mwaka kuwa na kundi la watu hawa ambao hawana ajira hivyo tumeangalia namna ya kumaliza tatizo hili,” alisema.
Alisema moja ya mambo yanayopaswa kufanyika ni serikali kuweka mikakati ya kuzalisha ajira pamoja na sekta binafsi.
Alisema ili kukabiliana na tatizo hilo, katika ripoti yao wamependekeza elimu inayotolewa shuleni ilenge kuwawezesha watahiniwa kujiajiri zaidi kuliko kuajiriwa.
“Pia kuna tatizo la watu wanaotoka vyuoni kutokuwa na sifa ya kuajirika… ni vyema sasa serikali ikahakikisha kuwa inaweka stadi za kuwawezesha wahitimu kusoma kile kinachofanyika kazini,” alisema.
Dk. Kiyondo, alisema pia serikali inatakiwa kuondoa vikwazo vya uwekezaji kwa wazawa na wageni kutoka nje kwa maana ya kulegeza masharti , sheria na kanuni za usajili wa kampuni mpya ili kuongeza uwekezaji nchini.
Alisema pia taasisi binafsi, zinatakiwa kutoa mafunzo kazini kwa wanafunzi walioko vyuoni ili kuwawezesha wanaohitimu kuwa na sifa za kuajiriwa.
Dk. Kiyondo, alisema sera ya ajira ya mwaka 2012 bado inamapungufu kwa sababu haijamsadia mwanamke kuingia kwenye soko la ajira.
Alisema kuhusu tatizo la ajira za utotoni, alisema wameishauri serikali kutekeleza sheria zilizowekwa ili kuwachukulia hatua wale wanaokuika masharti na kuajiri watoto.
“Pia ni vyema watu kupita majumbani ili kukagua na kuwaondoa watoto walioko kwenye ajira ili kumaliza tatizo hili,” alisema.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!