HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) bado inakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa damu, huku ikiwaomba viongozi wa dini, serikali na jamii za kimataifa kuhamasisha waumini na wananchi kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji.
Aidha, hospitali hiyo inakabiliwa na uhaba wa vitanda kwa ajili ya kukusanyia damu, usafiri wa kuwafuata wananchi katika maeneo mbalimbali, uhifadhi wa damu salama na vipimo vya kupimia damu.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Mwakwaiya Makani aliyasema hayo wakati alipokutana na Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing aliyekwenda kuchangia damu ikiwa ni maadhimisho ya siku ya uchangiaji damu duniani ambayo huadhimishwa Juni 14 ya kila mwaka.
Alisema MNH inahitaji jokofu kubwa la kibaiolojia kwa ajili ya kuhifadhia damu salama, kwani yaliyopo hayatoshi.
Ameishurukuru Serikali ya China akiitaja ni mdau muhimu hasa katika ujenzi wa Taasisi ya Upasuaji Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyoiwezesha serikali kupunguza rufaa za kupeleka wagonjwa nje ya nchi.
Akizungumza kabla ya kuchangia damu, Balozi Dk Youqing alisema jambo kubwa lililomsukuma kuchangia damu ni kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji wa damu ikiwemo wanaopata ajali, wanaofanyiwa upasuaji na wagonjwa wa saratani.
Naye Mkuu wa JKCI, Profesa Mohammed Janabi amepongeza hatua ya balozi huyo kujitolea damu ili kuokoa maisha ya watu wengine kwa kuwa damu ni changamoto kubwa hasa katika upasuaji.
Mahitaji ya damu hospitali hapo ni kati ya chupa 100 na 130 kwa siku, lakini damu inayokusanywa kwa siku ni kati ya chupa 60 na 100.
No comments:
Post a Comment