TPC yaahidi sukari kuingia sokoni Jumamosi
HATIMAYE Kiwanda cha uzalishaji sukari cha TPC cha Moshi, mkoani Kilimanjaro, jana kimeanza rasmi uzalishaji wa bidhaa hiyo ili kukabiliana na uhaba.




Kimeahidi kuwa bidhaa hiyo itaingia sokoni ifikapo Juni 18. Ofisa Mtendaji Mkuu na Utawala wa TPC, Jaffari Ally alimweleza hayo, Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Said Mecki Sadiki, wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kutembelea kiwanda hicho juzi.
“Tumeongeza asilimia 10 ya uzalishaji wa sukari kwa msimu huu, baada ya kuwa tumefanya uboreshaji na uwekezaji wa Dola 500.5, uwekezaji tulioufanya utasaidia kuwapo kwa sukari ya kutosha, kwa kuwa kwa siku moja tutazalisha tani 450,” alisema.
Aidha, alisema kwa msimu huu TPC itazalisha tani 106,000 na kuifanya mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara, kujitosheleza kwa sukari.
“Mkoa wa Kilimanjaro unahitaji tani 100,000, Arusha tani 100,000 na Manyara tani 70, tumepanga kuwa sukari ya ziada itakayozalishwa itasambazwa katika mikoa ya Tanga na Singida,”alisisitiza.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Mecki Sadiki, akizungumza mara baada ya kukitembelea kiwanda hicho alisema: “Nawashukuru kwa maandalizi mazuri ya kuanza msimu mpya, lakini nitoe onyo kwa wafanyabiashara, wasambazaji na wauzaji wa rejareja wauze sukari hiyo kuanzia Juni 18, kwa bei elekezi na wakiuza kwa bei ulanguzi, tutawakamata.”
Kwa miezi kadhaa, changamoto ya uhaba wa sukari imeonekana kuwa tatizo kubwa hapa nchini kutokana na kuadimika sokoni, baada ya viwanda vya ndani kuwa katika msimu wa kufanyia viwanda matengenezo kwa muda wa miezi mitatu.
Kwa kawaida viwanda hivyo, huanza msimu mpya kuanzia mwezi Machi hadi Juni ambayo ni kipindi cha miezi tisa ya uzalishaji.