Sunday, 26 June 2016

Sampuli ya sumukuvu kupimwa Marekani






Dar es Salaam. Idadi ya watu wanaohisiwa kuathirika kwa sumukuvu imeongezeka kutoka wagonjwa 21 hadi 32 na Serikali imeamua kupeleka sampuli mbalimbali za damu na vinyama vya ini kwenye maabara tofauti ikiwamo ya Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa cha Marekani (CDC).


Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema licha ya idadi hiyo kuongezeka, idadi ya vifo kutokana na ugonjwa huo imebaki kuwa saba, wakiwamo wanne wa familia moja.
Alisema watu walioathiriwa na ugonjwa huo wanaishi katika wilaya mbili za Chemba na Kondoa mkoani Dodoma na Serikali inaendelea na juhudi za kutambua kiini cha maradhi hayo kwa kupeleka jopo la wataalamu wa afya.
“Hadi jana (juzi) kulikuwa na jumla ya wagonjwa 12 ambao wanatibiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, 18 wanatibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kondoa, kati yao, 14 wamelazwa, miongoni mwao watano ni watoto. Watatu hali zao ni tete,” alisema. Waziri Mwalimu alisema sampuli mbalimbali zikiwamo damu, haja ndogo na kubwa, vinyama vya ini, sampuli za vyakula zimepelekwa katika maabara za Mkemia Mkuu wa Serikali, Maabara ya Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Maabara ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu na Maabara ya Hospitali ya KCMC.
“Vilevile, sampuli nyingine damu na haja ndogo zimepelekwa nchini Marekani katika maabara ya Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa cha Atlanta kwa ajili ya uchunguzi zaidi. Tunatumaini tutapata majibu ndani ya wiki moja kuanzia sasa,” alisema.
Waziri huyo alisema hadi sasa ni sampuli za nafaka pekee, zilizofanyiwa uchunguzi zilizoonyesha kuwapo kwa sumukuvu (aflatoxins).
“Jumla ya sampuli 13 kati ya 27 zilikuwa na uchafuzi wa sumukuvu kwa kiasi kisicho kubalika kwenye nafaka kwa mujibu wa viwango vya kitaifa na zote zilibainika kwenye mahindi. Sampuli 12 zilitoka Chemba, moja Kondoa,” alisema.
Alisema sampuli saba kati ya hizo, zilikuwa na kiasi kikubwa cha sumukuvu kiasi ambacho kiliwahi kusababisha madhara yatokanayo na sumu hiyo katika nchi za India, China na Kenya na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 120.
Waziri huyo alisema wameamua kuanza kuchukua tahadhari kwa matokeo hayo ya awali, huku wakiendelea kusubiri matokeo mengine na wameomba kitengo cha maafa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kuangalia jinsi ya kusaidia kupeleka nafaka katika wilaya hizo ili kukabiliana na athari zaidi.
Kuhusu dalili za ugonjwa huo, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Muhamad Kambi alisema mgonjwa hupatwa na kichefuchefu na kutapika, kuharisha damu, tumbo kuvimba na kujaa maji pia unashambulia na ini.
“Sumukuvu kama ilivyo jina lake ni sumu. Kutokana na kemikali zake kuwa na fungasi ambao hupatikana kwenye nafaka mbalimbali ikiwamo, karanga, uwele au mahindi ni hatari kwani humwathiri mgonjwa ndani ya saa 48,” alisema Profesa Kambi.
SUMUKUVU NI NINI?
Sumukuvu ni aina ya sumu inayotokana na fangasi wanaokuwa katika mazao ya nafaka au mazao yanapohifadhiwa.

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!